11 May 2012

Hospitali ya Agakhan kutoa tiba bure



Na Stella Aron

WANANCHI wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao bure ili kuzuia na kutibu magonjwa mbalimbali yanayoangamiza jamii kwa asilimia kubwa.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Agakhan Bi. Loveluck Mwasha, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya siku ya uuguzi duniani, ambayo huadhimishwa Mei 12, kila mwaka.


Alisema katika kusherehekea siku hiyo uongozi wa hospitali hiyo umeazimia kutoa huduma ya upimaji bure kwa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu kesho katika ukumbi wa Mlimani City.

"Tumechagua magonjwa hayo kutokana na watu wengi kupoteza maisha kwa kutofahamu dalili za magonjwa hayo kwa kushindwa kupata huduma za matibabu, " alisema Bi.Mwasha.

Bi.Mwasha alisema siku hiyo watatoa ushauri mbalimbali kwa watu warefu au wafupi na wenye uzito mkubwa namna ya kupunguza uzito ili kuepukana na ugonjwa wa shinikizo la damu na magonjwa mengine nyemelezi.

Alisema wananchi watakaogundulika kuwa na magonjwa hayo watatakiwa kwenda kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma zaidi, ambapo hivi sasa kuna idadi kubwa ya watu wanaougua magonjwa hayo lakini hawajitambui.

"Kwa wastani wa mwezi Agakhan tunapokea wagonjwa 50 wa kisukari ambao hupata tiba na kurejea majumbani mbali ya wale wanaolazwa," alisema Bi. Mwasha.

Muuguzi huyo alisema kabla ya kusherehekea siku hiyo uongozi wa hospitali hiyo jana ulitoa mafunzo kwa wauguzi wake namna ya kufuata maadili ya kazi na utoaji wa chanjo.

"Tumetoa mafunzo kwa wauguzi wetu ili waweze kukumbuka na kufuata maadili ya kazi zao na utoaji wa ushauri kwa jamii kufahamu umuhimu wa chanjo, " alisema.

No comments:

Post a Comment