28 May 2012
Wananchi warudisha imani ATCL-Chizi
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Ndege nchini ATCL Bw. Paul Chizi amesema idadi ya abiria wa shirika hilo imezidi kuongezeka baada ya wananchi kuonesha uzalendo na imani kwa kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi huyo ilieleza hatua hiyo inatokana na mpango walionao wa kujizatiti ili kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa anga kupitia mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa shirika hilo.
Bw. Chizi alisema tangu uzinduzi wa safari za Dar es Salaam-Kilimanjaro-Mwanza wiki moja iliyopita kwa kutumia ndege ya aina ya Boeing 737-500, kampuni yake imekuwa ikijaza abiria takribani 106 katika kila safari kwa siku tatu mfulilizo hali ambayo inaashiria kuwa wananchi wameanza kuwa na imani na huduma zinazotolewa na shirika lake.
“Ndege yetu kwa takribani siku tatu zilizopita imekuwa ikijaza abiria katika safari zote za Dar es Salaam-Kilimanjaro-Mwanza . Sikujua kuwa tutakuwa na uwezo wa kurejea na kupata mapokezi ya namna hii kwa haraka kutokana na kuwa kuna watoa huduma wengine katika njia hii,"alisema Bw.Chizi.
“Baada ya wananchi kuonesha imani na uzalendo,tutaendelea na kuongeza nguvu zetu katika kutoa huduma zetu kwa wakati na kwa bei nafuu. Nawaomba wananchi kuendelea na uzalendo wanaouonesha kwa faida ya kampuni yetu na nchi nzima kwa ujumla,” aliongeza.
Bw. Chiza alisema kuwa kurudi kwa huduma za ndege ya ATCL kumeanzisha vita ya viwango vya bei za usafiri wa anga baada ya ATCL kutoza bei ya chini kwa safari zake kunadaiwa kusababisha watoa huduma wengine wakiwemo Precision Air nao kupunguza gharama zao ili kukabiliana na ATCL.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment