28 May 2012

Taifa Stars, Malawi zaingiza mil. 40/-



Na Mwandishi Wetu

MECHI ya kirafiki ya kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Malawi (The Flames), imeingiza sh. 40,980,000 kutokana na mashabiki 9,365 walioingia uwanjani.

Mechi hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kujiandaa na mechi zao za kuwania kucheza Kombe la Dunia 2014 ambapo Stars itacheza na Ivory Coast Juni 2, mwaka huu na Malawi itaumana na Uganda.

Timu hizo ziliumana juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mapato hayo yametokana na hao waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 51,000 na sh. 20,000.

Alisema asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni sh. 6,251,186 ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa tiketi (sh. 4,999,800), waamuzi (sh.,105,000), usafi na ulinzi (sh. 2,350,000), maandalizi ya uwanja (sh. 400,000), Wachina (sh. 2,000,000) na umeme (sh. 300,000).

Aliongeza kwa upande wa mgawo asilimia 20 ya gharama za mechi ni sh. 4,714,803, asilimia 10 ya uwanja sh. 2,357,401, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 1,178,701, asilimia 20 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 4,714,803 na asilimia 45 ya TFF (sh. 10,608,306).

No comments:

Post a Comment