28 May 2012
Viongozi wapya Yanga Julai 15 *Mwesigwa apewa 'mikoba' kwa muda
Amina Athuman na Zahoro Mlanzi
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeitaka Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Yanga, ianze mchakato wa kujaza nafasi zilizo wazi kuanzia Juni Mosi, mwaka huu na Julai 15 ifanye uchaguzi wa viongozi wapya.
Hatua hiyo ya Kamati ya Uchaguzi imekuja baada ya kujadili kwa kina mustakabali wa uongozi ndani ya klabu hiyo pamoja na kupokea ushauri kutoka kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi kwa Wachezaji ya shirikisho hilo kutokana na kujiuzulu kwa Wajumbe nane na kifo cha Mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratias Lyatto alieleza kwamba katika kikao chao kilichofanyika jana jioni kiliamua Kamati ya Uchaguzi Yanga ifanye mambo matano muhimu.
Taarifa hiyo iliainisha mambo hayo ni kwamba kamati hiyo ianze mara moja mchakato wa kujaza nafasi zilizo wazi kwa wajumbe wa kuchaguliwa waliojiuzulu kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba ya Yanga.
"Mchakato huo uanze Juni Mosi kwa kuzingatia kikamilifu kanuni za uchaguzi wa uanachama wa TFF na uchaguzi wenyewe ufanyike Julai 15, mwaka huu mahali patakapopangwa na kamati hiyo na Sektetarieti ya klabu hiyo," ilieleza sehemu ya taariaf hiyo.
Ilifafanua zaidi kwamba Mkutano Mkuu utakuwa na agenda moja ambayo ni kujaza nafasi za viongozi hao wa kuchaguliwa na pia kamati hiyo iandae na kusimamia shughuli za uchaguzi kwa kuishirikisha sekretarieti chini ya kanuni za wanachama wa TFF kwa mujibu wa katiba ya TFF ibara ya 49(1) na katiba ya Yanga ibara ya 45(1) na (2).
Wakati huohuo, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imekabidhi shughuli zote za Klabu ya Yanga kufanywa na Sekretarieti ya Yanga chini ya Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa.
Kamati hiyo pia imewataka wajumbe wote wa klabu hiyo ambao hawajajiuzulu kutofanya shughuli zozote za klabu hadi nafasi za viongozi wa klabu hiyo waliojiuzulu zitakapozibwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Alex Mgongolwa, alisema nafasi za viongozi waliojiuzulu zitajazwa katika mkutano wa kawaida wa Yanga.
Alisema maamuzi hayo yamefanywa na kamati hiyo baada ya kukaa kikao na Kamati ya Utendaji Mei 26, mwaka huu na kutoa mwongozo kwa Yanga baada ya Kamati ya Uchaguzi Yanga kuomba mwongozo huo.
Alisema baada ya kupata taarifa rasmi kutoka Yanga, Kamati imebaini kuwa Kamati ya Utendaji ya Yanga imekosa akidhi baada ya wajumbe wake wengi kujiuzulu hivyo kutokuwa na uwezo wa kufanya uamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 32(1) ya Katiba ya klabu hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment