28 May 2012

Sherehe Simba yafunika Dar Live *Makalla aipa mtihani



Na Speciroza Joseph

NAIBU wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha ya Klabu ya Simba, amewataka wana-Simba kuendeleza umoja na mshikamano ili waendelee kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

Mbali na hilo, pia wafanye haraka kuwa na uwanja wao wenyewe wa kisasa zaidi ya ule unaomilikiwa na timu ya Azam FC kwani timu hiyo ina historia kubwa nchini.

Kauli hiyo aliitoa jana jioni wakati wa sherehe za kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao timu hiyo uliupata zilizofanyika katika Ukumbi wa Dar Live, Dar es Salaam.

Akizungumza na wanachama na mashabiki wa Simba waliojitokeza katika sherehe hizo, Makalla alisema Simba ni timu kubwa na inatakiwa kupiga hatua kubwa tofauti na ilivyo hivi sasa.

"Simba ina historia kubwa haikutakiwa kuwa katika hali hiyo, Serikali inajikita kukuza michezo kwa kuongeza walimu wa ndani wa kuendeleza mchezo huo uwe na mafanikio zaidi kwa wachezaji wa ndani," alisema Makalla.

Kabla ya Makalla kuzungumza, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu' aalisema ubingwa wao umetokana na ushirikiano wa wapenzi, wanachama na kuahidi watatengeneza timu bora zaidi ushindani ligi kuu na Klabu Bingwa.

Alisema baada ya arobaini ya aliyekuwa mchezaji wao, Patrick Mafisango kupita watafanya sherehe kubwa Watanzania wote.

Naye aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda alisema mwezi ujao anatarajia kutoa kitabu maalum kitakachoelezea historia ya Simba tangu ilivyoanzishwa na mafanikio iliyopata.

Alisema kitabu hicho kimechapishwa nje ya nchi ili kiwe na ubora zaidi ambapo anawaomba wanachama wao wakae mkao wa kula kusubili kitabu hicho.

Sherehe hizo zilipambwa na burudani mbalimbali ambapo Bendi ya Msondo Ngoma ndio ilikuwa ya kwanza kupanda jukwaani baada ya michezo ya watoto kumalizika na burudani zingine ziliendelea.

Vikundi mbalimbali vya ngoma na wasanii wa bongofleva walitoa burudani ya aina yake lakini iliyokonga nyoyo za watu wengi ni burudani kutoka kwa Bendi ya Taarab ya Mashauzi Classis iliyo chini ya msaniii, Isha Mashauzi.

No comments:

Post a Comment