14 May 2012

Vijana Yanga wamuangukia Manji


Na Elizabeth Mayemba

VIJANA wa Klabu ya Yanga, wamemuangukia aliyekuwa Mfadhili wa timu hiyo, Yusuph Manji aje kuinusuru hasa katika kipindi hiki kigumu walichonacho.

Klabu hiyo hivi sasa ipo katika mvutano mkubwa kati ya uongozi uliopo madarakani chini ya Llody Nchunga ambaye Baraza la Muafaka la Wazee pamoja na vijana wa klabu hiyo wanashinikiza kiongozi huyo kujiuzulu kutokana na kudai ameshindwa kuiongoza timu.


Wakizungumza kwa niaba ya vijana wenzao katika kikao cha vijana kilichofanyika jana Dar es Salaam ambacho kilihudhuriwa na zaidi ya wanachama 200, Omari Chambuso (003850), Hussein Mfaume (00607) na Waziri Jitu (001732), walisema wanataka Mkutano Mkuu ufanyike Mei 20, mwaka huu badala ya Julai 15 kama alivyotangaza Nchunga.

Walisema tarehe hiyo waliyopanga ndiyo tarehe ambayo Nchunga atakutana na Wazee wote wa Yanga na kwamba kama ana uwezo wa kukutana na wazee wote ni bora uwe mkutano mkuu kabisa.

"Nchunga amepanga Mkutano Mkuu ufanyike Julai lakini ni mbali sana, hivyo sisi tunataka ufanyike Mei 20 na pili tunataka ajiuzulu yeye pamoja na uongozi mzima," walisikika wakisema kwa nyakati tofauti.

Pia walimuomba Manji arudi kuisaidia klabu hiyo kwani uongozi uliopo madarakani wamedai umeshindwa kuiongoza timu hiyo kutokana na kukabiliwa na madeni mengi.

Waliongeza watajihidi vijana kwa umoja wao kuhakikisha wanajipanga kusaidia katika suala zima la usajili hususani katika kipindi hiki ambacho timu yao inakabiliwa na mashindano ya Kombe la Kagame.

No comments:

Post a Comment