18 May 2012
Usajili vikundi vya kahawa kuleta mafanikio kwa mkulima
Na Kassian Nyandindi
SERIKALI imekuwa ikisisitiza wakulima wanaozalisha mazao ya aina mbalimbali kuanzisha vikundi ambavyo wakijiunga kwa pamoja wataweza kuuza mazao yao kwa urahisi bila kurubuniwa na wafanyabiashara wajanja.
Vikundi hivyo ambavyo husisitizwa kuvisajili kisheria ili viweze kutambulika, kuwa na nguvu ya kukopesheka kutoka katika taasisi mbalimbali za kifedha kama vile benki.
Kuwaelimisha wakulima katika hili, ni suala ambalo wataalamu wa sekta husika walipewa kulikeleza kwa vitendo, kuhakikisha kwamba wakulima wanaozalisha mazao ya biashara wanapewa kipaumbele katika kuelimishwa juu ya umuhimu wa kujiunga pamoja ambapo baadaye ni ukombozi mkubwa kwao.
Wakulima wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameitikia wito wa kuanzisha vikundi ambavyo sasa vimesajiliwa chini ya wizara ya katiba na sheria (RITA) ili kupata haki zao za msingi.
Vikundi 55 wilayani hapa vinavyozalisha kahawa vimekabidhiwa vyeti vya usajili, ili waweze kuuza kahawa yao moja kwa moja mnadani Moshi na hata kwa minada ya nje ya nchi.
Jitihada hizo ni wazo lililotolewa kwa mara ya kwanza na Mbunge wa Mbinga Mashariki Bw. Gaudence Kayombo, kwa lengo la kumwezesha mkulima wa zao hilo, aweze kuuza kahawa yake moja kwa moja mnadani na sio kupitia makampuni binafsi.
Mchango huu uliotolewa na Mbunge huyu ni wa kuungwa mkono kwani utaweza kumsaidia mkulima hata kupata malipo ya kahawa yake kwa bei ya uhakika, sio kama ilivyokuwa kwa miaka nyuma ambapo hakunufaika na chochote katika kilimo cha zao hilo kutokana na wafanyabiashara wajanja kumuibia.
Bw. Kayombo ameviunganisha vikundi hivyo ili viweze kupata mkopo wa fedha kwa kila kikundi, za kununulia kahawa kavu katika msimu wa mavuno ya zao hilo unaotarajiwa kuanza Julai Mosi mwaka huu.
Mikopo hiyo itatolewa kwa vikundi ambavyo vitakidhi vigezo vya kukopesheka kulingana na dhamana walizonazo ambazo benki itaridhia.
Usajili huu unavifanya vikundi viweze kutambulika, kuwa na nguvu ya kisheria katika utendaji wa kazi zao za kila siku, hali ambayo itawafanya waweze kuboresha zao la kahawa na kuongeza thamani ya uzalishaji.
Katika sherehe za kukabidhi vyeti vya usajili kwa vikundi hivyo zilizofanyika hivi karibuni katika kijiji cha Linda kata ya Linda, Ofisa Maendeleo ya Jamii Bw. Paschal Ndunguru ambaye alikuwa akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, anasema ni fursa ya kipekee kwa wanavikundi hao kufanya hivyo kwani kutawawezesha kufanya shughuli zao za uzalishaji kwa viwango vinavyotakiwa.
Bw. Ndunguru anasema, ili waweze kuwa endelevu wanapouza kahawa na kupata malipo, wanakikundi wanatakiwa wawe na nidhamu nzuri katika matumizi ya fedha na sio kuzitumia hovyo katika masuala ya anasa, badala yake wanunue pembejeo za kuendeleza zao hilo na kufanya maendeleo mengine ikiwemo kupeleka watoto shule.
“Ninawasihi tuachane na anasa za dunia hii, tuzingatie kupeleka watoto wetu shule na kufanya mambo mengine ya kimaendeleo katika maisha yetu”, anasisitiza.
Amevishauri, vikundi hivyo kuweka mfumo mzuri wa mapato na matumizi katika kikundi husika, ili kuepukana na malalamiko yasiyo ya lazima miongoni mwao.
“Ndugu zangu tuwe tunajituma katika kazi na kujenga dhana ya kidemokrasia katika kufanya vikao mara kwa mara ndani ya vikundi, hali ya uchumi hivi sasa sio nzuri vijana tuhakikishe tunajituma katika uzalishaji hususani kwenye kilimo”, anasema Bw. Ndunguru.
Anasema, halmashauri ya wilaya hiyo katika bajeti ya mwaka huu, imejiwekea mikakati kuhakikisha kwamba zao la kahawa linaboreshwa kwa kiwango cha juu, ikiwemo kuwaelimisha wakulima juu ya utunzaji na upuliziaji wa madawa ya kuua wadudu aina ya vidung’ata ambavyo vimekuwa vikishambulia zao hilo kwa kasi.
"Maisha bora hayawezi kuja kama watu tunakuwa na umaskini wa mawazo, hivyo binadamu kujituma katika kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo ndio msingi wa kupiga hatua katika maisha" anasema.
Pamoja na mambo mengine wakulima hao wameshauriwa kwenda katika vituo vya afya au hospitali kupima afya zao mapema, ili waweze kujitambua kama wana magonjwa watibiwe mapema na hatimaye wasiweze kupoteza nguvu kazi ya taifa hili, katika kuendeleza kilimo cha kahawa.
Wahenga husema kilimo ndio uti wa mgongo, hivyo kinachotakiwa sasa ni kuendelea kujituma ili kuhakikisha wanayafikia malengo waliyojiwekea.
Katika maeneo mengi nchini na duniani kilimo, huchangia maendeleo ya mahali husika kwa kiasi kikubwa, endapo tu kanuni bora za kilimo zikifuatwa katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Sasa yatupasa katika kuyasemea haya tunataka kuone utekelezaji kwa njia ya vitendo, na sio wataalamu kuendelea kukaa maofisini na kufanya kazi kwa mazoea katika mafaili tu, wakati mkulima aliyekuwa kijijini anasubiri huduma kupitia utaalamu hao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment