02 May 2012
Ubadhirifu mali za umma wachelewesha mishahara
Na Florah Temba, Kilimanjaro
IMEELEZWA kuwa vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma, ufisadi na wizi kwa baadhi ya watumishi na viongozi ni moja ya sababu inayoifanya Serikali kukosa mapato hivyo kushindwa kupandisha mishahara ya wafanyakazi.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Leonidas Gama wakati akizungumza na wafanyakazi mkoani humo katika siku ya wafanyakazi iliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Ushirika na Stendi ya Biashara Moshi na kuongozwa na kauli mbiu isemayo 'Mishahara duni, Kodi Kubwa na Mfumuko wa Bei ni Pigo kwa wafanyakazi'.
Bw. Gama alisema kimsingi mishahara ya wafanyakazi ni midogo na haitoshi lakini inasababishwa na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya watendaji na viongozi kutokuwa waaminifu hivyo kujihusisha na vitendo vya rushwa na wizi wa mali za umma.
Alisema, vitendo vya baadhi ya viongozi na watumishi kujiingiza kwenye rushwa na wizi wa mali za umma vimechangia kwa kiasi kikubwa serikali kukosa mapato na hivyo kushindwa kupandisha mishahara ya wafanyakazi.
Alisema, baadhi ya wafanyakazi na viongozi kutokuwajibika kikamilifu katika kutekeleza wajibu wao, kuwepo kwa rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu inachangia kwa kiasi kikubwa wafanyakazi kupata mishahara midogo.
“Baadhi ya viongozi kutowajibika ipasavyo, kujiingiza kwenye wizi, rushwa, ubadhirifu, ufisadi vinachangia kwa kiasi kikubwa serikali kukosa uwezo wa kutoa mishahara mikubwa kwa wafanyakazi...sasa tubadilike tuwajibike ipasavyo ili kukuza uwezo wa serikali kimapato na kuiwezesha kutoa mishahara inayokidhi haja za wafanyakazi,” alisema Bw. Gama.
Alisema, sababu nyingine inayochangia mishahara duni kwa wafanyakazi ni kudorora kwa uchumi wa Dunia kuanzia mwaka 2009 pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Akizungumzia suala la mfumuko wa bei Bw. Gama alisema linasababishwa na kuendelea kuwepo kwa biashara za magendo ambapo watumishi wa serikali wanahusika.
“Suala la mfumuko wa bei kwa kweli ni tatizo na hili pia linasababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo kuendelea kukithiri kwa biashara za magendo na katika hili watumishi wanahusika kwani katika mipaka ni sisi watumishi tuko lakini pia uzalishaji mdogo katika viwanda vyetu na mazao pia ni tatizo,” alisema Bw. Gama.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment