Na Queen Lema, Meru
KATIKA hali isiyo ya kawaida, mkazi wa Kijiji cha Nkoanekoli, Kata ya Nkoaranga, mkoani Arusha Bi. Martha Joseph (77), ameuawa na wananchi wenye hasira na kuchomwa moto akituhumiwa kijihusisha na vitendo vya kishirikina.
Akizungumza na Majira jana, Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Elipokea Palangyo, alisema mbali ya mauaji hayo nyumba yake aliyokuwa akiishi pia ilichomwa moto.
Alisema tukio hilo limetokea jana saa nne usiku baada ya bibi huyo kuonekana akimshika kijana mmoja mkazi wa kijiji hicho sehemu mbalimbali za mwili wake.
Baada ya muda, kijana huyo alipatwa na maumivu makali ya mwili ambayo yalisababisha ndugu zake wamchukue na kumpeleka nyumbani kwa bibi huyo.
Walipofika na kueleza wasiwasi wao, bibi huyo aliwahakikishia ngugu kuwa maumivu hayo yatapungua baada ya muda mfupi hivyo aliwataka waondoe hofu na kurudi nyumbani.
“Ngugu wa kijana huyu waliondoka hadi nyumbani kwao lakini baada ya muda mfupi, maumivu yaliongezeka hasa sehemu ya tumbo hivyo ndugu zake waliamua kumrudisha kwa bibi wakiamini pengine alimfanyia vitendo vya kishirikina.
“Walipofika nyumbani kwa bibi huyu, ndugu zake walijichukulia sheria mkononi kwa kumpiga wakidai ni mchawi na baada ya muda alipoiteza maisha kutokana na majeraha aliyopata sehemu mbalimbali za mwili wake,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, uongozi wa kijiji hicho ulitoa taarifa polisi ili kwenda kumuokoa ambapo askari walipofika eneo la tukio, walikuta mwili huo ukiwa kwenye tairi ukiungua taratibu.
“Polisi walipofika eneo la tukio, waliutoa mwili huo kwenye moto ili usiungue zaidi na kubaki majivu pamoja na kuwatawanya wananchi waliochukua sheria mkononi,” alisema Bw. Palangyo.
Aliongeza kuwa, polisi hao pia walifanikiwa kuzima moto uliokuwa ukiteketeza nyumba ya bibi huyo ambayo ilichomwa moto na wananchi wenye hasira.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Thobias Andengenye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, uchunguzi unaendelea.
Tukio la watu kuchukua sheria mikononi mwao linafaa lishtumiwe na likomwe. Hata ingawa kazi ya ushirikina ni hatia haifai kwa vyovyote vile kuchukua sheria mikononi mwetu na kulipiza kisasi. Kuna taasisa za serikali ambazo zimebuniwa kushughulikia mambo kama haya
ReplyDelete