16 May 2012
Ubabe sio suluhu ya kumaliza mgomo
Na Grace Ndossa
JUZI mgambo wa Manispaa ya Ilala walimzuia Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Gabriel Fuime kuingia ofisini na wafanyakazi wake wakishinikiza kusikilizwa madai yao.
Askari hao waligoma kufanya kazi kwa wiki tatu ili kushinikiza manispaa hiyo kuwalipa madai yao ya msingi ya muda mrefu ndipo waweze kuingia katika mkataba mpya.
Wanamgambo hao walieleza kuwa, wameitumikia Manispaa hiyo kwa zaidi ya miaka kumi bila kupewa ajira za kudumu na kubaki kuwatumia kwa faida zao binafsi.
Walieleza kuwa walipoanza kazi katika manispaa hiyo walianza kwa mikataba ya muda mfupi walipoamaliza mikataba hiyo waliingia mkataba mwingine mipya ambayo mpaka leo hawajapewa stahiki zao.
Madai mengine ni marekebisho kiwango cha shilingi elfu 4000 kwa siku wanachopewa ambacho ni kidopgo hivyo kuhitaji viwango vinavyolingana na maisha ya sasa.
Walieleza kuwa wamechoshwa kugeuzwa vibarua wa muda mrefu na madai yao ya msingi yanashindwa kutekelezwa kwani wanahitaji mikataba inayofuata sheria za kazi ambapo mwaka jana waliahidiwa kuongezewa mishahara lakini hadi leo hakuna kilichofanyika.
Cha Kushangaza walikaa muda wa wiki moja kushinikiza uongozi wa Manispaa hiyo kuwapa malimbikizo na kuboresha mikataba yao kutokana na kazi ngumu wanazozifanya na vikwazo wanavyokumbana navyo kila siku.
Askari hao hufanya kazi mbali mbali za Manispaa na kuhakikisha hakuna wafanyabiashara wanaouza bidhaa katika sehemu zisizo rasmi na kuondoa wamachinga katika maeneo yasiyoruhusiwa.
Kitendo cha Manispaa hiyo kukaa kimya kwa muda mrefu bila kutatua matatizo ya askari hao ni cha dharau kwani inaonesha wazi kuwa wanawatumiwa bila malipo na kupoteza nguvu zao.
Pia kitendo cha kutolewa kauli ambazo siyo nzuri kwa wafanyakazi hao sio cha kiungwana kwani viongozi hao wanatakiwa kujua kwamba Cheo ni dhamana na usipokitumia vizuri kinaweza kukuletea matatizo.
Nionavyo kitendo cha kuchelewa kusikilizwa na kujibiwa kuwa wao walikuwa vibarua tu na hawakuwa na mikataba ya ajira katika kufanya kazi kwani wana askari wa kutosha kufanya kazi walizokuwa wanazifanya hakikuwa cha kiungwana.
Kama kweli walikuwa na askari wa kutosha kufanya hizo kazi kwanini wawatafute mgambo hao kwenda kuwafanyia kazi na wengine wamepoteza hata meno yao kwa kupambana na wahalifu katika jiji hilo na bila hata kuwapatia fedha za matibabu.
Pia nashindwa kuelewa kwamba hata Mkurugezi wa Manispaa hiyo alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alijibu na kueleza kwamba walikuwa ni vibarua tu kwani hataka kama mtu akiwa kibarua si anatakiwa kupewa kilicho chake na kuelezwa kwamba kwa sasa hatutahitaji tena vibarua hadi hapo kazi zitajitokeza.
Manispaa hiyo kwa dharau bila kuwaita na kuwaeleza wanatoa tangazo kwenye ubao wa matangazo wanaeleza kuwa askari hao sii wanamgambo tena wa manispaa hiyo hicho siyo kitendo cha uungwana lazima wawe na utu na hofu ya mungu katika maamuzi yao.
Kauli hizo zilizaa mgogoro uliodumu kwa wiki tatu wakati wangetumia muda mfupi kumaliza mgogoro huo.
Pia walipaswa kuwapa haki zao hata kama walishindwa kuwalipa wale waliopata adha katika sehemu ya kazi kwani wengine hawana meno kabisa kutokana na vuta nikuvute katika sehemu zao za kazi.
Viongozi wakumbuke kuwa viapo walivyoapa katika kufanya kazi wafanye kwa uaminifu kwani kabla ya kupata kazi hizo unawakuta wakijinadi kwa wananchi kwamba watatatua matataizo ya wananchi yanayowakabili lakini wakishapata madaraka wanasahau kabisa.
Ikumbuke kuwa hizo nafasi walizonazo wanatakiwa wawe wakarimu na kuwa na lugha nzuri kwa wafanyakazi ili hata kama huna fedha za kumlipa leo wala kesho aweze kuwa na matumaini na siyo kutoa maneno ya kashfa .
Viongozi wa namna hiyo ni wale ambao hawatakiwi katika jamii kwani wanashindwa kutumia mamlaka waliyonayo kuzungumza na wafanyakazi kero zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi, wakae wakijua kwamba kutumia ubabe siyo suluhu ya matatizo.
Hata hivyo viongozi wengi wanasubiri matatizo yakishakuwa makubwa ndiyo wanakaa chini na kulitafutia ufumbuzi badala ya kutatua pale mwanzoni linapotokea.
Hawa ndiyo viongozi wetu wanaotuongoza kwani tatizo lishakuwa kubwa ndiyo wanakumbuka kuwa kuna kukaa chini katika meza ya mazungumzo na kufikia muafaka, kweli tukienda hivyo hatuwezi kufika sehemu yoyote.
Hata kwa msingi wa kufikia utawala bora hatutafika kwani serikali inapompa mtu dhamana ya kuongoza katika eneo lolote anajua uwezo wa kuongoza anao lakini anapofika pale anajua akitumia lugha ya kibabe ndiyo atafanikiwa.
Kiongozi yoyote ukipewa dhamana ya kuongoza lazima uwe na lugha laini ya kuongea na wafanyakazi na kuhakikisha kuwa mahusinano na mawasiliano mazuri katika sehemu ya kazi ili wafanyakazi waliopo waweze kuwajibika ipasavyo.
Pia anapaswa kutambua kuwa kiongozi mzuri ni yule anayekaa na wafanyakazi na kuzungumza nao, kushaurina na wafanyakazi na siyo kuchukua maamuzi yake mwenyewe kama avyoelewa, pia kuondoa nafasi iliyoachwa wazi kati ya wafanyakazi na viongozi wao pamoja na kutumua elimu yake aliyoanayo kuhamasisha wafanyakazi wawajibike ipasavyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment