17 May 2012

Tume ya kukusanya maoni ipewe ushirikiano


Na Darlin Said

TUME ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba mpya hivi karibuni imeanza kazi tangu ilipoapishwa na Raisi Jakaya Kikwete.

Wakati wanaapishwa raisi Jakaya Kikwete moja ya ahadi  iliyoitoa kuwa bega kwa bega ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na tija na kupatikana kwa maoni ya wananchi ambayo ndio chachu ya katiba itakayojenga Tanzania mpya.


Tume hiyo yenye wajumbe 30 kutoka Tanzania bara na Visiwani tayari imeshakabidhiwa jengo maalum na magari 30 zikiwemo nyumba kwa wale waishio nje ya Dar es salaam.

Kazi kubwa ya Tume hii ni kusimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya Katiba ili watanzania waweze kupata katiba mpya ambayo itakidhi na kukata kiu yao.

Majukumu mengine ya tume hiyo ni pamoja na kukusanya maoni, kuyachambua na kuandika rasimu ya katiba ambayo itazaa katiba mpya.

Pia kuhakisha elimu inatolewa  ya kutosha kwa wananchi kuhusu katiba ili wawe na ufahamu na uhuru wa kutoa maoni bila ya kukwazwa kuzuiwa au kutishiwa.

Wakati huohuo Tume imepewa jukumu zito la kuakikisha kwamba wanafanya kazi kwa hali na mali ili kuwatendea haki watanzania na baadaye kufikia hatima ya kile kanachohitajika kwa maslahi ya nchi.

Wakati wanakabidhiwa ofisi aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Bi.Celina Kombani alisema tume imepewa kazi nzito isiyohitaji ubaguzi wa aina yeyote ambao inahitaji uaminifu, nguvu, maarifa na uvumilivu.

Hivyo basi italazimika kufanya kazi katika mazingira magumu usiku na mchana kwa ajili ya wananchi na taifa kwa ujumla

Katika makabidhiano hayo Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba alivitaka vikundi na wananchi waliopendekeza majina ya wajumbe wa tume  kuiacha huru ifanye kazi iliyopewa.

Hivyo waliopendekeza majina ya wajumbe hawa wasitarajie kuwa wajumbe watafanya watakayo wao kwani tume hiyo ni ya watanzania wote na si watu wachache

Nionavyo, kauli ya Jaji Warioba ya kutaka wawe huru ilikuwa na dhamira nzuri lakini  bado kauli hiyo inachangamoto  kubwa kwani  inaweza kutafasiriwa kuwa tume itapenda iachwe iandike Katiba ya watanzania bila kusukuma na mtu yeyote.

Uundaji wa katiba ni nguzo na ujezi wa muafaka wa kitaifa na hakuna makubalino yanayoweza kupatikana bila msukumo wa wananchi.

Ingawaje tume imetaka iwe huru lazima muwasikilize wananchi kwa kupokea maoni yao bila ya upendeleo wowote ili iweze kutenda haki na kahakikisha watanzania wanashiriki mchakato huo.

Kwa kufanya hivyo mtaweza kuleta katiba mpya ambayo itaijenga Tanzania mpya yenye usawa katika nyanza  zote za kisiasa, kimila na utamaduni, bara na visiwani pamoja na usawa dini.

Tunawaamini na kuwategemea kwani mchakato huu ni muhimu na nyeti kwa mustakabali wa taifa, bila katiba iliyo bora hatuwezi kuijenga Tanzania iliyo safi.

Aidha ili muweze kufahamu watanzania wanahitaji nini lazima mtoe elimu ya kutosha ili waelewe umuhimu  wa wao kushiriki.

Kwa kukafanya hivyo mtawasaidia wananchi kuwa na ufahamu na uhuru wa kutoa maoni bila ya kukwazwa kuzuiwa au kutishiwa.

Kwani Watanzania waliowengi hasa waishio vijijini  bado hawajui katiba nini  na wala  hawajui umuhimu wake kwao, hivyo elimu kwao ni muhimu kabla ya kuomba maoni yao.

Mwenyekiti wa Tume na wajumbe wako muelewe kwamba tume hiyo  ni nguzo ya mchakato wa katiba mpya waipendayo watanzania.

Ndani ya miezi 18  mliyopewa kukamilisha zoezi hilo ni imani ya watanzania muundo wa katiba inayokuja itakuwa imeboreshwa mazuri, imeondoa mapungufu ili kujipima tulikotoka na tuendako.

Naamini  wajumbe wote wa tume wana sifa na uwezo mkubwa kiasi kwamba kama watazingatia misingi mikuu ya uundaji wa Katiba Mpya na ya Kidemokrasia inaweza kufanya kazi hiyo nzuri.

Aidha nawapongeza  na kuwatakia kila la kheri  wajumbe wote waliochaguliwa kulitumikia taifa letu  kwa kusimamia na kuakikisha kuwa Watanzania wanapata katiba mpya ambayo itakidhi mahitaji yao.

Ni rai yangu kwa wananchi kujitokeza na kuwapa ushirikiano watakapohitaji ili kurahisiha mchakato wa kupata katiba mpya kwa maendeleo ya nchi yetu.

No comments:

Post a Comment