Na Raphael Okello, Bunda
WAKAZI wa Kitongoji cha Buzige, Kijiji cha Mulanda, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, juzi walishangazwa na tukio la mbweha mmoja na tumbili wawili waliowaua na kuchomwa moto lakini walishindwa kuungua na kutoweka kusikojulikana.
Baada ya tumbili hao kupata kipigo kabla ya kuuawa, waligaragara chini kama binadamu na kunyoosha juu miguu yao kama ishara ya kuwasihi wananchi wasiuchome moto mzoga wa mbweha ambaye ndiye alitangulia kuuawa na wananchi hao.
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao waliwaua tumbili hao, kuchukua mizoga yao na kuiweka pamoja na mbweha.
Walichukua kuni, kumwagia mafuta ya taa na kuwasha moto ambao ulishindwa kuunguza mizoga hiyo wala kuonesha dalili ya kuungua.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya
Namhula Bw. Boniphace Manyonyi, alisema tukio hilo limetokea juzi kijijni hapo baada ya wanyama hao kujeruhi baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho.
Alisema siku ya tukio, mkazi wa Kitongoji hicho Bw. Muyenjwa Zakayo, alimuua mbweha ambali alipambana naye kuanzia usiku hadi alfajiri kwa kwa kumchoma mkuki baada ya kuingia nyumbani kwake katika mazingira ya kutatanisha.
Alisema mbweha huyo alimjeruhi vibaya mtoto wake, Nezia Muyenjwa (11), ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mulanda sehemu mbalimbali za mwili akiwa amelala na wenzake.
Bw. Zakayo alisisitiza kuwa, katika harakati za mapambano na mbweha huyo, wananchi walifika nyumbani kwa Bw. Zakayo na kufanikiwa kumuua.
“Wakiwa katika harakati za kuchoma mzoga wake, ghafla walitokea tumbili wawili ambao walianza kulia kwa huruma na kugaragara chini kama binadamu.
“Tumbili hawa walinyoosha miguu yao juu ikiwa ni ishara ya kuwasihi wananchi wasichome moto mzoga huo, wananchi waliamua kuwaua tumbili hawa ambao hawakuwa na dalili ya kutishika na mauti,” alisema.
Aliongeza kuwa, imani ya wananchi wanyama hao wangekimbia badala yake walibaki eneo hilo hadi mauti ilipowakuta wakiendelea kunyoosha miguu.
Wananchi waliamua kuchimba shimo na kuwafukia wanyama hao lakini muda mchache baadaye walikuta kaburi hilo likiwa wazi na wanyama hao hawako hali iliyowapa wananchi wasiwasi.
Hili ni tukio la pili kutokea katika kitongoji hicho ambapo mwishoni
mwa Machi mwaka huu, mbweha aliyeuawa na wananchi baada ya kumvamia Bw. Mugeta Makanga, mzoga wake kushindwa kuungua moto na kaburi alilofukiwa kukutwa likiwa wazi.
No comments:
Post a Comment