17 May 2012

TIC yasifu ushiriki wa UNIDO




Na Nyakasagani Masenza

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesifia ushirikiano mkubwa kinaoupata kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) katika kuhamasisha uwekezaji nchini.

Pongezi hizo zilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw. Raymond Mbilinyi, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya taasisi hizo mbili za uwekezaji Afrika 2011 na taarifa ya ufuatiliaji wa hali ya uwekezaji iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.


"Uhusiano kati ya TIC na UNIDO ni wa muda mrefu tangu mwaka 2000, tunatarajia kuwa tutaendelea hivyo ili kuhamasisha uwekezaji endelevu hapa nchini," alisema Bw. Mbilinyi.

Alisema kwa msaada wa UNIDO, umewezesha kituo hicho kuhakiki miradi iliyosajiliwa na TIC na kuthibitisha kwamba karibu asilimia 80 ya miradi hiyo inafanya kazi.

Aliongeza kuwa kupitia UNIDO, kituo hicho kiliweza kuendesha mafunzo ya kuendeleza biashara nchi nzima na kusaidia kuendeleza miradi 400 ambapo miradi 80 ilichaguliwa na kuendelezwa zaidi na kuifanya iweze kukopesheka, kutafutiwa masoko na kuunganishwa na wadau wengine ndani na nje ya nchi.

"UNIDO imeendelea kuisaidia TIC katika kujenga uwezo wa wafanyakazi wake hadi sasa," alisema.

Kwa upande wake, mwakilishi wa UNIDO  nchini, Bw. Emmanuel Kalenzi, alitoa shukrani zake kwa kwa TIC kwa kuongoza taasisi nyingine kwa niaba ya serikali katika utafiti huo wa masuala ya uwekezaji.

Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Mary Nagu, alisema ingawa Tanzania imeweza kuvutia mitaji ya uwekezaji toka ndani na nje ya nchi, bado haijaweza kufahamika hasa ni miradi mingapi inafanya kazi vizuri na ni thamani kiasi gani imeingiza kwenye uchumi.



No comments:

Post a Comment