24 May 2012

TFF watakiwa kutoa mafunzo kwa wataalum mashuleni



Na Mwali Ibrahim

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeombwa kutoa nafasi za mafunzo ya michezo kwa wataalamu wa michezo katika Shule za Msingi na Sekondari ili kukuza viwango vya wataalamu hao waweze kuibua vipaji zaidi.

Maombi hayo yalitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bishop Durning (Bishop Durning High School) ya Arusha Sarubare Lendisa, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi habari kuhusiana na umuhimu wa michezo shuleni.


Lendisa alisema michezo mashuleni inakabiliwa  na changamoto nyingi hivyo kusababisha kushindwa kukidhi haja ya kuibua vipaji zaidi.

Alisema changamoto zipo nyingi, lakini kubwa ni TFF kushindwa kutoa nafasi za wataalamu waliopo katika shule kuhudhuria kozi zinazotolewa na TFF, kwa ajili ya kusaidia kuibua vipaji, kwani inaonesha vipaji vingi hukomazwa badala ya kuibuliwa na kutunzwa kitaalamu.

"Naililia TFF kutoa kozi kwa walimu wetu kwakuwa tunapokosa walimu wataalamu tunashindwa kuibua na kutunza vipaji," alisema

Alizitaja changamoto nyingine ni pamoja na shule nyingi zenye michepuo ya michezo kutokuwa na uwezo wa kuhimili gharama za kununua vifaa vya michezo ambavyo ni chachu ya michezo.

Sambamba na hayo aliiomba Serikali kutoa mkazo wa kuimarisha michezo mashuleni, ikiwa ni pamoja na kuibua vipaji vya michezo inayoonekana kusaulika katika mashule ikiwemo mchezo wa ngumi ambao kwa muda mrefu umekuwa hauchezwi katika shule mbalimbali nchini na badala yake kuacha katika majeshi pekee.

Lendisa alisema shule yake ni moja ya shule zinazoibua vipaji bila kuathiri taaluma nyingine, na tayari imeshashiriki michuano mikubwa ya kitaifa ambapo hivi karibuni pia wamepata mwaliko wa kwenda nchini Burundi kushiriki mchezo wa mpira wa miguu kwenye sherehe za uhuru wa nchi hiyo baada ya kupata mwaliko kutoka taasisi ya Rolling stone.

No comments:

Post a Comment