02 May 2012

TB changamoto - Dkt.Mungure


Na Mohamed Hamad Manyara

KASI ya maambukizi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) wilayani Kiteto mkoani Manyara imezidi kuongezeka kutokana na Ukimwi kuongezeka kwa asilimia 2.6, imeelezwa.

Hayo yalielezwa jana na Dkt. Willycharles Mungure Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi na Huduma Shirikishi za Ugonjwa wa Kifua Kikuu wilayani Kiteto wakati akizungumza kwenye kikao na Kikundi cha Watoa Elimu juu ya magonjwa hayo.

Dkt. Mungure alisema ongezeko la watu wanaougua ugonjwa wa kifua kikuu linazidi ambapo sasa jumla ya watu 265 wilayani humo kati Januari hadi Desemba, mwaka 2011 walibainika na kuendelea na tiba ya ugonjwa huo.

“Kasi hii ni kubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo walikuwa chini ya idadi hiyo na kwamba inazidi kuongezeka kutokana na ongezeko la ugonjwa wa Ukimwi hapa nchini,”alisema Dkt. Mungure na kuongeza kuwa.

“Pamoja na changamoto hiyo, idara tumekuwa na mikakati mbalimbali katika kukabiliana nayo ikiwemo ile ya kutokomeza kabisa ugonjwa huu ambao ni tishio la maisha ya watu,” aliongeza.

Pia alitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kutoa huduma shirikishi za kifua kikuu na Ukimwi, kupunguza makali ya maisha ya mgonjwa mwenye kifua kikuu na Ukimwi, pamoja na kupunguza watu wenye TB na Ukimwi wasiambukizwe tena.

Katika hatua nyinginge mratibu huyo alieleza kuwa wameanzisha bodi ya kushughulikia magonjwa hayo pamoja na vikundi vya watu 60 waliowahi kuugua ugonjwa wa kifua kikuu na kupona ambao wanafanya kazi ya kuelimisha jamii.

No comments:

Post a Comment