30 May 2012
Serikali yabainika kuchelewesha vitabu vya bajeti 2012 na 2013
Na Godfrey Ismaely, Dar es Salaam
ZIKIWA zimebakia siku chache kabla ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingia katika vikao vya Bajeti, mwaka wa fedha 2012 na 2013 baadhi ya wanaharakati wamedai kusikitishwa na uwajibikaji mdogo wa Serikali hasa kuchelewa kutoa vitabu vya makadirio hayo.
Kwa mujibu wa Ibara ya 96 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la mwaka 2007) wabunge wanapaswa kupokea vitabu vya makadirio ya bajeti ya Serikali angalau siku 21 kabla ya kikao cha Bunge la bajeti kuanza.
Pamoja na kwamba kikao cha bajeti kinatarajia kuanza Juni 12, mwaka huu hadi Mei 29, 2012 tafiti zinaonesha bado wabunge walikuwa hawajapokea nyaraka hizo muhimu na haijulikani ni lini watazipokea.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Taasisi ya Sikika na kusainiwa na Mkurugenzi wake Bw. Irenei Kiria ilieleza kwamba hatua hiyo inatia wasiwasi katika utendaji.
"Tumesikitishwa na hatua ya Serikali kushindwa kutoa vitabu vya makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013, siku 21 kabla ya kikao cha Bunge la Bajeti kuanza, jambo ambalo ni ukiukwaji wa Kanuni za Kudumu za Bunge.
"Hii ni kinyume na kanuni na maazimio mbalimbali yaliyoridhiwa na serikali likiwemo, Tamko la Dar es Salaam la mwaka 2011 lililotolewa na wananchi na Azaki karibu 100 kutoka nchi mbalimbali duniani na mashirika 12 ya Kimataifa," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, tamko hilo linasisitiza uwazi katika bajeti, uwajibikaji na ushirikishwaji kwa kuzitaka Serikali Kuu na serikali za mitaa kutengeneza na kujadili waziwazi katika muda mwafaka angalau nyaraka nane muhimu za bajeti ambapo kati ya nyaraka hizo mojawapo ni makadirio ya bajeti.
Pia kutolewa kwa wakati kwa vitabu vya makadirio ya bajeti vya mwaka wa fedha unaofuata kwa wabunge na umma kwa ujumla ni hatua muhimu katika kuongeza uwazi, ubora wa bajeti na ufanisi wa ushiriki wa wabunge katika kikao cha kujadili na kuidhinisha bajeti.
Taasisi ya Sikika, ilibaini kuwa ni kawaida kwa wabunge kupokea vitabu vya bajeti kwa kuchelewa na wakati mwingine huvipata baada ya kikao cha bajeti kuanza.
"Hali hiyo pia inaweza kusababisha wabunge kupitisha bajeti bila kufahamu undani wa kile wanachokijadili au kupitisha bajeti isiyo na tija wala kipaumbele kwa taifa," iliongeza taarifa hiyo.
Pamoja na kuchelewa kupatiwa vitabu vya makadirio ya bajeti, Sikika pia imebaini kuwa wabunge hupatiwa vitabu vya makadirio ya bajeti toleo la I-IV ambavyo kwa kawaida huwasilisha jumla kuu za vifungu bila maelezo ya kina.
"Na huwa hawapatiwi kabisa Vitabu vya Muundo wa Matumizi vya Muda wa Kati ya Bajeti (MTEF) kwa kila Wizara, Idara na Mashirika mbalimbali ambavyo ndivyo hubeba maelezo ya bajeti na shughuli zitakazotekelezwa," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
"Sikika imekuwa ikipitia tovuti ya Wizara ya Fedha, Bunge na kubaini kuwa hadi leo (jana) tarehe 29, Mei 2012 vitabu vya bajeti kwa mwaka wa fedha 2012/13 havijawekwa kwenye tovuti hizi mbili," iliongeza taarifa hiyo.
Aidha, tafiti zinaonesha kuwa hali hiyo inawanyima wabunge pamoja na wananchi fursa ya kushiriki kikamilifu katika mjadala wa kuichambua bajeti kabla ya kuidhinishwa na Bunge.
Pia tatizo hilo lilijidhihirisha mwaka jana (2011) ambapo wabunge hawakupata vitabu hivyo kwa wakati mwafaka.
"Sikika inatoa rai kwa Serikali kuhakikisha inatoa vitabu vya bajeti, mwaka wa fedha 2012/13 toleo la I-IV na vitabu vya Muundo wa Matumizi ya Muda wa Kati (MTEF) kwa kila Wizara, Idara na mashirika mbalimbali kwa wabunge kabla ya kuanza kwa kikao cha bajeti. Hii itawapa wabunge muda wa kufanya uchambuzi wa kina na kushiriki kikamilifu katika mjadala na hatimaye kuidhinisha bajeti yenye manufaa kwa wananchi," ilifafanua taarifa hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment