30 May 2012

Posta waanzisha duka la kununua, kubadilisha fedha za kigeni Dar



Na Sangalwise Abia, Dar es Salaam

SHIRIKA la Posta Tanzania limefungua biashara ya kuuza na kununua
fedha za kigeni (Bureau de change) katika ofisi zake zilizopo Posta
Mpya Mtaa wa Azikiwe jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ni kati ya mikakati ya shirika hilo ambayo inalenga kuhakikisha linawapatia wateja wake nchini kote huduma mbalimbali zenye tija na ufanisi, kibiashara zikiwa mahali pamoja ili kuwapunguzia kutumia muda mwingi wa kuzitafuta mbali.

Meneja Masoko wa shirika hilo Bw. David George aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na gazeti hili juu ya mipango mikakati ya shirika ambayo inalenga kuboresha huduma zake nchini kote.

Alisema, walifikia hatua hiyo baada ya kupewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania hivi karibuni.

"Lengo la kuanzisha huduma hii ni kwamba tunahitaji kuhakikisha Watanzania wanapata huduma mahali pamoja badala ya wateja kuhangaika huku na kule wakitafuta huduma. Kwa hali hiyo sisi posta tukaliona hilo...hivyo tukaamua kuanzisha huduma hiyo,"

"Lengo letu ni kwamba mteja anapoingia katika Ofisi za Posta basi ategemee kupata huduma mbalimbali, hatua hiyo itawasaidia wateja kutopoteza
muda mwingi kwa kutafuta mahitaji,” alisema Bw. George.

Alisema, kwa sasa Shirika la Posta limeshaanzisha huduma nyingi
zikiwepo huduma za Posta Cash, EMS Courier, EMS Cargo, Post Cargo City
urgent mail (pCUM), huduma ya Internent Cafe na sasa huduma ya
kuuza na kununua fedha.

"Hayo yote yakiwa ni malengo ya kusogeza huduma za kibiashara karibu zaidi na jamii ili huduma hizo zipatikane kwa urahisi na mahali pamoja badala ya kutafuta huduma sehemu mbalimbali," aliongeza.

Bw. George alitoa mwito kwa wateja kuhakikisha wanatembelea katika Ofisi ya Posta ili wajipatie huduma ya Posta Bureau de Change sambamba na huduma
nyinginezo za shirika hilo kwa kuwa zinatolewa kwa ufanisi wa hali ya juuikiwemo gharama nafuu zaidi.

No comments:

Post a Comment