29 May 2012
Pamba yaondoka na matumaini kibao
Na Daud Magesa, Mwanza
MABINGWA wa zamani wa soka Tanzania Pamba ya Mwanza, imeondoka jijini hapa ikiwa na matumaini makubwa ya kufuzu fainali za Kanda ili kucheza Ligi Daraja la Kwanza.
Pamba ambao ni mabingwa wa soka Mkoa wa Mwanza, iliondoka juzi kwa basi la kukodi ikiwa na kikosi cha wachezaji wake wote chini ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhan Muzzo na kuahidi ushindi.
Wadau wa soka jijini hapa ambao walifika kuwaaga wachezaji wa timu hiyo, makocha na viongozi, walisema silaha pekee itakayowasaidia kufuzu katika michuano hiyo ni nidhamu kwa kila mchezaji na kutimiza majukumu yao.
Wadau hao waliwataka wachezaji wa timu hiyo iliyowahi kutikisa soka la Tanzania katika miaka ya 1980 na mwishoni mwa 1990, kuwakilisha vyema mkoa na kubwa ikiwa ni kupata nafasi ya juu ili kufuzu kucheza Ligi Daraja la Kwanza.
Walisema wakishikamana na kufuata maelekezo ya makocha na wakizingatia nidhamu katika michuano hiyo ni wazi watafanya vizuri.
"Kikubwa ni kuzingatia nidhamu, kuonesha mshikamano wenu kama timu uwanjani na nje ya uwanja, kila mchezaji atimize wajibu wake pamoja na changamoto mliyonayo ya ukata," alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Waandishi wa Habari ya Kuhamasisha Pamba ishinde, Mashaka Baltazar
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) Jackson Songora, alisisitiza nidhamu kwa wachezaji hao akisema mkoa huo upo pamoja nao kuhakikisha wanafanya vizuri.
Pamba iko katika Kituo cha Kigoma pamoja na wenyeji JKT Kanembwa, Majimaji ya Tabora, Mwadui ya Shinyanga, Mabingwa wa Mkoa wa Singida, CDA ya Dodoma na Bandari ya Kagera.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment