29 May 2012
Airtel yakabidhi vifaa vya michezo kwa DRFA
Na Elizabeth Mayemba
KAMPUNI ya simu za mikononi ya Airtel Tanzania imekabidhi vifaa vya michezo kwa timu za vijana chini ya miaka 17 zitakazoshiriki mashindano ya Aitel Rising Stars, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho katika mikoa sita.
Mikoa ambayo itashiriki michuano hiyo ni Lindi, Mbeya, Arusha, Ilala, Temeke na Kinondoni, ambapo kwa upande wa Ilala mechi zitakuwa zikichezwa Uwanja wa Airwing, Kinondoni Mwenge na Temeke mechi zitachezwa Uwanja Twalipo.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Sanifu Kondo, Afisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde, alisema jumla ya timu 24 zinatarajiwa kushiriki mashindano hayo.
Alisema vifaa vilivyotolewa ni jezi na mipira na kila timu itapatiwa jezi mbili.
"Mwaka huu tumeboresha zaidi michuano hii ikiwa ni pamoja na kushirikisha timu za wasichana tofauti na hapo awali, ambapo kila mkoa utatoa timu ya wanawake ambayo itakuwa kombaini.
"Mwaka huu mashindano yatashirikisha mikoa sita kwa kuanzia ngazi ya mikoa kabla ya ile ya taifa itakayoanza Juni na timu bingwa itashiriki mashindano ya siku nne nchini Kenya yajulikanayo kama Inter Continental Tourmament yatakayoshirikisha mataifa zaidi ya 16," alisema Jane.
Alisema mbali na timu hiyo pia watateua wachezaji sita bora ambao watashiriki kliniki ya soka maarufu kama Coaching Stars itakayofanyika nchini Kenya chini ya jopo la makocha kutoka Academy ya soka ya Manchester United ya Uingereza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment