22 May 2012
Ofisa Usalama afariki dunia
Na Lilian Justice, Morogoro
MWENDESHA pikipiki anaedaiwa kuwa Ofisa Usalama Manispaa ya Morogor mkoani Mrogoro amefariki dunia baada ya kugongana na mwendesha pikipiki mwenzake huko katika maeneo ya Mizani Kihonda katika manispaa hiyo.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani hapa Bi. Adolphina Chialo alisema tukio hilo lilitokea Mei 19, mwaka huu majira ya saa 11.30 jioni huko katika maeneo ya Mizani Kihonda mjini hapa.
Bi. Chialo alisema pikipiki yenye namba za usajili T 699 BFU SUNLG amabayo ilikuwa ikiendeshwa na Bw. Richard Feliciana (35) mkazi wa Chamwino mjini hapa ilikuwa ikitokea Mkundi kuelekea mjini na iligongana na pikipiki nyingine yenye namba za usajili T 281 AQU Honda iliyokuwa ikendeshwa na Bw. Singoli Elia, ambaye alifariki dunia na kudaiwa alikuwa Ofisa Usalama na mkazi wa Forest.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, marehemu alikuwa akitokea maeneo ya mjini kuelekea Mkundi na chanzo cha ajali hiyo kinachunguzwa zaidi.
Hata hivyo, taarifa za awali za Kikosi cha Usalama Barabarani kimebaini chanzo cha ajali hiyo ni marehemu kuendesha pikipiki yake kulia zaidi mwa barabara.
Wakati huohuo, mtembea kwa miguu amefariki dunia mara baada ya kugongwa na gari mali ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mjini hapa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro Bi. Adolphina Chialo, tukio hilo lilitokea Mei 18 mwaka huu, majira ya saa 12.30 jioni huko maeneo ya Magubike wilayani Kilosa.
Bi. Chialo alisema gari lenye namba za usajili SU 36224 Toyota Land Cruiser ikiendeshwa na Bw. Kassim Urasa (53) mkazi wa Kihonda, ilikuwa ikitokea Mkoani Singida na ilimgonga mtembea kwa miguu Emanueli Godfrey (7), mwanafunzi wa darasa la Kwanza katika Shule ya Msingi Magubike na kufariki dunia papo hapo.
Hata hivyo, Kamanda huyo alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva na uchunguzi zaidi unaendelea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment