22 May 2012

Ndugu wakamatwa na nyara za Serikali



JESHI la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia wakazi wawili ambao ni ndugu katika maeneo ya Kihonda Kilimanjaro Manispaa ya Morogoro mkoani humo kwa kosa la kukutwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Akizungumzia tukio hilo jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Bi. Adolphina Chialo alisema lilitokea Mei 19, mwaka huu, majira ya saa 9.00
alasiri huko maeneo ya Kihonda mjini hapa.


Alieleza kuwa askari waliokuwa doria waliwakamata Bw. Omari Mohamedi (56), mkazi wa Kilimahewa na Bw. Salumu Mohamed (52) mkazi wa Nunge ambao ni wanandugu wakiwa na ngozi za chui nne kinyume cha sheria huku wakiwa wamezipakia kwenye baiskeli.

Hata hivyo, Kamanda huyo alisema watuhumiwa hao wamekamatwa na thamani ya ngozi hiyo bado haijafahamika kwani uchunguzi maalumu bado unasubiriwa kutoka Idara ya Maliasili kuhusiana na tukio hilo ili kuweza kufanya tathimini halisi ya ngozi hizo.

Wakati huo huo imeelezwa Mei 19, mwaka huu majira ya 12.45 jioni huko maeneo ya Melela, Wilayani Mvomero, mkazi wa eneo hilo Bw. Bakari Rombo (29) ambaye ni mfugaji alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu kuibwa kwa ng'ombe wake
watano wenye thamani ya sh. milioni 2.5 wakiwa zizini.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Bi. Adolphina Chialo alisema chanzo cha tukio hilo kinachunguzwa na mpaka sasa hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment