17 May 2012

Mradi wa kuzuia maji ya bahari wakwama


Na Mwajuma Juma,
Zanzibar

MRADI wa kuzuia maji ya baharini ili yasiingie katika makaazi ya
wananchi umeshindwa kutekelezeka baada ya fedha zilizoombwa
kukamilisha mradi huo kutowafikia walengwa.



Hayo yameelezwa na Mwakilishi  jimbo la Kikwajuni Bw. Mahmoud Mohammed
Mussa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia
ofisi za viongozi wakuu wa kitaifa wakati alipofanya ziara kwenye
maeneo ya Binguni na Maisara Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.


Bw. Mussa alisema kuwa kabla ya kuanzishwa mradi huo wananchi
waliiomba jumla ya shilingi milioni 780 Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa lengo la kutekeleza mradi huo.


Hata hivyo alisema kuwa ofisi hiyo ilituma shilingi milioni 531 lakini
hazijuulikani wapi zilipofikia na kuwa zinatarajiwa kuundiwa mradi
mwingine jambo ambalo wananchi hawakubaliani nalo.


“Kimsingi mradi umeshindwa kutekelezeka na tunachohoji wapi fedha hizo
zimekwenda,” alisema Mwakilishi huyo.


Alisema kuwa kutokana na kuwepo uvumi huo kinachotakiwa kujuulikana
fedha hizo zimetumwa wapi ili wananchi hao waweze kuendeleza azma yao.


Tunajua fedha zimetumwa lakini wapi hatujui na kama zipo ni kwanini
utafutwe mradi mwingine wakati walioomba ni wananchi wa jimbo la
Kikwajuni hii kwa kweli sio sawa,” alisema.


Hata hivyo akizungumza mbele ya kamati hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Idara
ya Mazingira Bi. Sihaba Haji Vuai alisema kwamba kiasi hicho cha fedha
kinasubiriwa ili kutengeneza maeneo ya malindi ambayo kuna njia
imekatika.


No comments:

Post a Comment