16 May 2012
Mkomanzi yadaiwa kutoa ahadi hewa
Na Yusuph Mussa, Kilimanjaro
WANANCHI wa Kijiji cha Muheza, Kata ya Maore wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro wamesema Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi bado haijaweza kuwasaidia huduma za jamii, kama shule, zahanati, maji pamoja na kuahidi kufanya hivyo baada ya kupandishwa hadhi kutoka pori la akiba.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) tawi la Muheza Bw. Samwel Mmbaga kwa Mwenyekiti
wa Baraza la Vijana wa chama hicho Taifa Bw. John Heche alipofika
kulizindua tawi hilo.
"Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi walituahidi kutusaidia huduma za jamii,
pindi hifadhi hiyo itakapoanza, lakini hadi leo hawajatusaidia lolote
iwe ujenzi wa zahanati, madarasa ya shule au maji.Lakini pia hifadhi
hii ya Mkomazi imechukua maeneo makubwa ya mbuga na kufanya sehemu ya
kulisha mifugo yetu kuwa ndogo," alisema Bw. Mmbaga.
Bw. Mmbaga aliiomba Serikali kuboresha huduma za mifugo kwa kuwajengea
mnada wa mifugo yao, lakini pia kuboresha kilimo kwa kujenga bwawa la
umwagiliaji, huku wakitaka huduma za maji safi na salama, lakini pia
akidai akina mama wanakwenda umbali mrefu kufuata zahanati.
Kada wa chama hicho Wilaya ya Same ambaye pia alikuwa mgombea ubunge
kwa tiketi ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu, mwaka 2010 Jimbo la
Same Mashariki Bi. Naghenjwa Kaboyoka alisema kukosa ubunge sio mwisho
wa kutatua matatizo ya wananchi.
"Hayo matatizo yenu nipeni miezi michache ijayo nioneshe kwa
vitendo. Mimi sio Mbunge wa kuzungumza bungeni, lakini ni Mbunge wa
wananchi, hivyo nipeni muda nianze kazi ya kutatua kero zenu," alisema
Bi. Kaboyoka.
Naye Bw. Heche aliwaasa wananchi kuikataa CCM kuanzia uchaguzi wa
vitongoji mwaka 2014 hadi Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, lakini matatizo
yote wanayopata ni kutokana na baadhi ya viongozi waandamizi wa
Serikali kukwapua rasilimali za wananchi bila huruma.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment