11 May 2012

Mjamzito ajifungulia lango la zahanati


Na Heri Shaaban

UONGOZI wa Kata Vijibweni iliyopo Kigamboni wamemuagiza Mganga Mkuu Zahanati ya Vijibweni, Bi.Rukia Msumi, kuagiza walinzi wa zahanati hiyo kuacha geti wazi ili wagonjwa waweze kuingia baada ya kutokea tukio la mjamzito kujifungulia getini.

Agizo hilo lilitolewa juzi wakati wa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na diwani huyo, Bw. Suleiman Methew akiongozana na wenyeviti wake. Alikemea vikali kitendo cha walinzi kukataa kufungua milango hadi mjamzito akajifungulia nje.

Bw. Methew alimtaka mganga mkuu awaagize walinzi wa hospitali hiyo kuruhusu magari kuingia ndani wakati wote.

Bw.Methew alisema baada ya kupata malalamiko ya makosa  yanayofanywa na walinzi wa zahanati hiyo kwa muda mrefu yeye kama kiongozi amekerwa.

"Wananchi wangu kufanyiwa vitendo vya aina hii sijaridhika navyo, kuanzia leo naomba magari yote ya wagonjwa yaingie ndani kama vituo vingine vya afya wanavyofanya pindi wanapopokea wagonjwa," alisema Bw.Methew.

Alimtaka mganga huyo kusimamia suala hilo ili vitendo vya aina hiyo visijirudie.

Kwa upande wake Mganga Mkuu, Bi.Rukia Msumi, alisema taarifa hizo zilimfikia na alitoa onyo lakini kampuni hiyo ya ulinzi ilipuuzia.

No comments:

Post a Comment