11 May 2012
Mchezaji wa zamani wa Man U azindua Airtel Rising Stars
Na Elizabeth Mayemba
KAMPUNI ya Simu za mikononi ya Airtel jana ilizindua awamu ya pili ya mpango kabambe wa mpira wa miguu nchini Airtel Rising, ambao nia yake ni kutafuta na kukuza vipaji vya mchezo huo kutoka ngazi ya chini kabisa mpaka ya taifa.
Michuano ya Airtel Rising Stars iliyozinduliwa na mchezaji wa zamani wa Manchester United Quinton Fortune, itaanza kutimua vumbi Mei 24 mwaka huu, kutoka mikoa sita, fomu za usajili zinapatikana kwenye makao makuu ya ofisi za Airtel Lindi,Mbeya,Arusha,Kinondoni, Ilala na Temeke.
Awamu ya kwanza ya mpango huu ilifanyika mwaka jana na kupata mafanikio makubwa, lengo likiwa ni kuvipika vipaji vinavyochipukia chini ya umri wa miaka 17, nafasi ya kuonyesha vipaji vyao kwa makocha waliobobea pia kupata nafasi ya kuendeleza vipaji vyao.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Sam Elangallor alisema, mafanikio ya mwaka jana yanaonesha mpira wa miguu una uwezo wa kuunganisha makabila mbalimbali na pia kuleta hamasa kwa jamii ya chini hadi taifa.
"Mwaka jana zaidi ya timu 11,000 Afrika zilijiandikisha kushiriki kwenye michuano hii kuanzia kwenye mtoano na kuchagua wachezaji ambao waliunda timu zilizoshiriki kwenye ngazi ya mkoa, ushiriki huu mkubwa ulituonesha ya kwamba tuko kwenye njia sahihi, na ndio maana tuna hamasa kubwa na awamu hii ya pili kwa mwaka huu," alisema Elangallor
Alisema kama ilivyokuwa kwa mwaka jana, mpango huu utaanzia ngazi ya mkoa na taifa na kufuatiwa na kliniki ya soka ya kimataifa chini ya wakufunzi kutoka klabu ya Manchester United ya Uingereza, kwa mwaka huu kutakuwa na mashindano ya siku nne ya timu bingwa kutoka kila nchi itakayoshiriki kushindania taji jipya la Airtel Rising Stars African Champion.
Kwa mwaka huu michuano hii imezinduliwa na mchezaji wa zamani wa Manchester United Quinton Fortune, mchezaji aliyesajiliwa na kocha Sir Alex Ferguson mwaka 1999 akitokea klabu ya Atletico Madrid wakati huo akiisaidia timu yake kushinda vikombe vitatu.
Raia huyo wa Afrika kusini aliweza kuzoea haraka mazingira wa Uingereza na kuweza kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha Ferguson kama winga wa kulia,kiungo wa kati na mshambuliaji, akiwa Man U Fortune aliiwezesha timu yake kushinda taji la FA mwaka 2003.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment