04 May 2012

Madiwani walalamikia fedha za maendeleo



Na Yusuph Mussa, Tanga

BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamesema fedha za miradi zinazopelekwa kwa wananchi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni kidogo ukilinganisha na kiwango kilichoidhishwa kwenye bajeti, hivyo madiwani hao kuonekana ni waongo mbele ya jamii.


Hayo yalisemwa jana kwenye mafunzo ya siku tatu kwa madiwani hao yanayoratibiwa na halmashauri kwa uwezeshaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambapo Diwani wa Kata ya
Mgwashi Bw. Bakari Kavumo alisema kutopeleka fedha hizo ni kuwahadaa wananchi.

"Kila tunapopitisha bajeti na Serikali kukubali kiwango cha fedha za kuleta kwenye halmashauri, Hazina haileti fedha hizo kwa wakati uliopangwa, lakini kibaya zaidi fedha zinaletwa kidogo tofauti na tulizoidhinishiwa kwenye bajeti," alisema Bw. Kavumo.

Diwani wa Kata ya Mtae Bw. Said Shehiza alisema madiwani bado hawajapewa meno ya kutosha kuwa walinzi wa fedha za halmashauri, kwani baadhi ya mikataba wao hawahusishwi.

"Madiwani tunaambiwa halmashauri ni yetu, lakini tumewekewa mipaka tunaambiwa
tusiingie jikoni, hivyo tunashindwa kujua kinachoendelea kwenye mambo mengi," alisema Bw. Shehiza.

Diwani wa Kata ya Mamba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Lushoto Bi. Zubeda Titu alisema falsafa ya CCM kuwa Diwani ni figa la tatu haina maana kwao, kwani figa hilo limeonekana kama ngazi tu ya kumuwezesha Mbunge na Rais kupata madaraka.  

"Figa la tatu ambalo ni sisi madiwani ni la kukanyagia ili mafiga mengine yapande. Diwani analipwa sh. 120,000 kwa mwezi, Mbunge pamoja na kulipwa mamilioni ya fedha bado akipewa uwaziri anafanya mambo ya kifisadi... Serikali ni lazima iangalie maslahi yetu na sisi madiwani," alisema Bi. Titu.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tanga Bw. Yohana Miwa
akitoa mada alisema Diwani ni mwakilishi wa wananchi, hivyo anatakiwa akutane mara kwa mara na waliomchagua ili kuchukua maoni yao na kuyafanyia kazi kwenye ngazi mbalimbali.

Akizungumza na mwandishi, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Dule- Bumbuli Bw. Sebarua Shemboza alisema Rais Kikwete amepiga 'Ikulu' baada ya kuwaondoa wakaguzi wa ndani kwenye halmashauri.

"Kama kuna jambo ambalo Rais Kikwete ameonesha nia ya dhati ya kufanya maboresho katika kudhibiti fedha za umma kutumika visivyo kwenye halmashauri ni kumuondoa Mkaguzi wa Ndani kuwa chini ya Mkurugenzi, hiyo itaongeza uwajibikaji na ulinzi wa fedha," alisema Bw. Shemboza.


No comments:

Post a Comment