23 May 2012

Lembeli: Kumuondoa Maige haikuwa kazi rahisi





Na Patrick Mabula, Kahama

MBUNGE wa Kahama, mkoani Shinyanga, Bw. James Lembeli, amesema kazi ya kumuondoa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Bw. Ezekiel Maige katika nafasi yake, haikuwa kazi rahisi.

Bw. Lembeli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Majengo mjini hapa.

Katika mkutano huo, wananchi walitaka kufahamu kwanini Bw. Lembeli hakutia saini azimio la baadhi ya wabunge kupiga kura ya kutokua na imani na Waziri Mkuu ili kushinikiza Mawaziri ambao Wizara zao zimeguswa na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wajiuzulu.

Akijibu swali hilo, Bw. Lembeli alisema kazi ya kupambana na jambo hilo ilikuwa ngumu kutokana na Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda kukataa ripoti ya kamati yake pamoja na mapendekezo waliyotoa isisomwe bungeni.

“Kimsingi nitakuwa mkweli daima katika mambo ya msingi yanayohusu maslahi ya Taifa, kupiga vita ufisadi na matendo maovu kwa kutumia nafasi mliyonipa, miaka saba mfululizo mnanichagua kuwa mbunge wenu nawashukuru sana,” alisema Bw. Lembeli.

Bw. Lembeli alisema, baada ya kubaini mizengwe hiyo alimfuata Bi. Makinda na kumwambia kama hataki ripoti yao isomwe bungeni yupo tayari kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa kamati hiyo.

“Nilimwambia Bi. Makinda kama hataki ripoti yetu isomwe bungeni nitajiuzulu uenyekiti kwani tumetumia zaidi ya sh. milioni 200 kuchunguza ufisadi ndani ya Wizara hii.

“Nikiwa bungeni na kamati yangu, watu walianza kusema tumehongwa pesa ili ripoti yetu isisomwe ndipo nilichukua uamuzi mgumu wa kuhakikisha inasomwa ili umma ufahamu yale ambayo tumeyaona katika uchunguzi wetu,” alisema.

Alisema isingependeza kuona kamati yao haitoi taarifa ya mambo ambayo tayari walikuwa wamemaliza uchunguzi wake na kujua yaliyokuwa yakifanyika lakini walikumbana na mizengwe.

Aliongeza kuwa, kama yeye anapenda pesa wakati huo fedha zilikuwa nje nje lakini matokeo ya ripoti yake yameonesha wazi jinsi kamati hiyo ilivyofanya kazi nzuri bila kununuliwa hivyo wakazi wa Kahama lazima wafahamu kuwa mbunge wao yupo makini.

Taarifa ya kamati hiyo ilichangia kumwondoa Bw. Maige ambaye pia ni Mbunge wa Msalala katika nafasi yake ambapo kuondolewa kwake kumepokelewa kwa hisia tofauti na wakazi wa Kahama hata kuleta mgawanyiko mkubwa kisiasa.

6 comments:

  1. Hivi mtu mzima anaulizwa kwa nini hakutia saini azimio la baadhi ya wabunge kupiga kura ya kutokua na imani na Waziri Mkuu ili kushinikiza Mawaziri ambao Wizara zao zimeguswa na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wajiuzulu.Atakuwa amejibu swali kweli kwa maelezo aliyo yatoa yanayo husu kamati yake?Kwa maoni yangu hajajibu swali kabisa.

    ReplyDelete
  2. hapa inaonyesha woga aliokuwa nao, kwani kama alikuwa amedhamilia aliktakiwa kuwa mkweli daima kwa kutia saini

    ReplyDelete
  3. Watu wa aina hii ni wengi sana na inatokana na kwamba nje ya ccm ni vigumu kutoka na wanaotoka ni wale tu waliokaribu na pia serikali na TRA unaambiwa kodi inayokusanywa aidha inaishia TRA au wafanyakazi wa serikali na ccm ndio mpambe yeye atafanya nini, watoto wasiende chooni haiwezekani. Dawa tutawaliwe na hata jiwe lakini sio ccm uenda na sisi tutatoka

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ni ukweli usiopingika kwamba mwaka 2015 wabunge wote ambao wanajifanya kuwa watetezi wa Wanyonge na hawakuweza kusaini ile karatasiya kutokua na imani na Waziri Mkuu ili kushinikiza Mawaziri ambao Wizara zao zimeguswa na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wajiuzulu wajiandae kujibu swali hili ipasavyo vinginevyo kutokusaini kwao kutawagharim.

      Delete
  4. Mimi naamini jasiri haachi asili, huyu anayeitwa `eti Mheshimiwa` Lembeli ni jasili katika utekelezaji wa majukumu ya wakuu wake wa kazi siyo mtetezi wa wanyonge,ikumbukwe kuwa wanyonge 90% wamevua `Gamba` wamevaa gwanda, sasa yeye anatetea wanyonge huku amevaa gamba ni mnafiki atakiona cha moto Twetytwelve

    ReplyDelete
  5. NDIO UMETUMIA MIZENGWE KUMNG'OA HUYO KIJANA MAIGE ILA NILISHANGAA PAMOJA NA WATU WENGI KUPENDEKEZA UTEULIWE UWAZIRI MBONA PATUPU HIVI UNATEGEMEA KURUDI TENA BUNGENI KWA TIKETI YA CCM NAKUFANANISHA NA BAADHI YA WABUNGE WALIOKUWA WAKISHUPALA UFISADI KAMA NGAZI YA KURUDI BUNGENI WENGI WALIOPITA KWA JUHUDI ZAO SASA NI MABUBU

    ReplyDelete