25 May 2012

Kibaha wahitaji fedha kupanua sekta ya afya




Na John Gagarini, Pwani

KITUO cha Afya wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani kinahitaji kiasi cha shilingi bilioni 13 kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho ili kuwa hospitali ya wilaya hiyo.

Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jana Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Dkt. Kaniki alisema kuwa tayari ujenzi huo umeanza.


Dkt. Kaniki alisema kuwa wamepeleka maombi maalumu serikalini kwa ajili ya ujenzi huo ambapo waliomba kiasi cha shilingi milioni 500 na kuwapatiwa shilingi milioni 290.

“Kiasi hicho cha fedha kilitolewa mwaka 2008 na 2009 ambazo zilitumika kwa ajili ya kujenga jengo la wagongwa nje yaani OPD, ” alisema Dkt. Kaniki.

Alisema kuwa, majengo ambayo yataongezwa ni jengo la wazazi na watoto wachanga, upasuaji mkubwa na akinamama, jengo la maabara, exray, wodi za wagonjwa wanawake na wanaume, jengo la magonjwa ya kuambukizwa jengo la kuhifadhia maiti na jengo la usafi.

“Mbali ya kupeleka maombi maalumu pia tumepeleka kwenye balozi za Korea Kusini kitengo cha misaada kwa huduma za afya na ubalozi wa Ireland ambako kote kwa bahati mbaya fedha hazikuweza kupatikana,” alisema Dkt. Kaniki.

Mganga Mkuu huyo wa halmashauri ya mji Kibaha alisema kuwa eneo la hospitali hiyo lina ukubwa wa hekari zaidi ya 10 na kuwataka wadau mbalimbali kujitokeza kufanikisha ujenzi huo.

Aidha aliwaomba wafadhili kujitokeza kuwasaidia ili waweze kufanikisha ujenzi huo ambapo michango imekuwa ni changamoto kubwa kufanikisha upanuzi huo ili kuisaidia Hospitali ya Tumbi ambayo itakuwa ya mkoa.


No comments:

Post a Comment