25 May 2012

Waziri awakabidhi bendera Twiga Stars


Na Mwali Ibrahim

NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makalla jana alikabidhi bendera ya taifa kwa timu ya taifa ya Wanawake ,Twiga Stars, kabla ya kuelekea Ethiopia kwa ajili ya Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC), zitakazofanyika Novemba mwaka huu, Equatorial Guinea.

Twiga Stars waliondoka nchini jana saa 11 jioni  kwa ndege ya Shirikia la Ndege la Ethiopia, kikosi hicho kikiwa na msafara wa watu 24 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi itacheza na Ethiopia katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya mchujo kwa ajili ya fainali hizo, ambapo mechi yao inatarajiwa kuchezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Addis Ababa, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye Dar es Salaam.

Timu ya Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa Ethiopia itakuwa imepata tiketi ya kwenda Equatorial Guinea.

Wachezaji walioondoka na kikosi hicho ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Ester Chabruma, Ettoe Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri, Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia Hamis, Semeni Abeid na Zena Khamis.

Kwa upande wa Benchi la Ufundi ni Charles Mkwasa (Kocha Mkuu), Nasra Mohamed (Kocha Msaidizi), Furaha Francis (Meneja wa Timu), Mwanahamisi Abdallah (Mtunza Vifaa) na Christina Luambano (Daktari wa Timu).

Twiga Stars ambayo msafara wake uliongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Lina Mhando itarejea nyumbani siku moja baada ya mchezo huo  saa 6 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.

Kabla ya mechi hiyo, Twiga walishajipima nguvu na mechi za kimataifa dhidi ya Zimbabwe na kufungwa mabao 4-1 na Banyana Banyana ya Afrika Kusini ambayo iliwafunga mabao 5-2.



No comments:

Post a Comment