14 May 2012
IFNA yashauri Taifa Queens icheze Kombe la Dunia
Na Amina Athumani
SHIRIKISHO la Kimataifa la Mchezo wa Netiboli (IFNA), limekipa Changamoto Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) kuiingiza timu ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) kwenye michezo ya Dunia.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mwakilishi wa IFNA, Joan Smith alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mchezo huo hususani kikosi cha Taifa Quens kilichoshiriki michuano ya Afrika kimeimarika tofauti na alichokiona mwaka 2009 katika mashindano kama hayo.
Alisema pia maandalizi yaliyofanywa na CHANETA kwa mwaka huu yamekuwa ni mazuri zaidi na kwamba chama hicho kina uwezo pia wakuandaa mashindano ya Dunia endapo watafanikiwa kuwa na Uwanja wa Ndani wa kisasa.
Alisema kutokana na maandalizi waliyofanya CHANETA, IFNA inao uwezo wa kuipa kibali Tanzania kuandaa mashindano ya Dunia na kwamba cha msingi ni Serikali ya Tanzania kukisaidia chama hicho katika kuhakikisha kinapata kiwanja cha ndani chenye hadhi ya kisasa.
Tanzania ni mara ya pili kuandaa michezo ya Afrika ambapo mara ya kwanza iliandaa michezo hiyo mwaka 2009 na iliiwezesha Tanzania kupanda viwango vya kimataifa vya mchezo huo vinavyotambulika na IFA.
Kwa sasa Tanzania ipo nafasi ya 20 katika viwango vya mchezo huo na ipo nafasi ya tatu kwa viwango vya Netiboli Afrika (AN) ambapo kupitia mashindano yaliyomalizika juzi huenda Tanzania ikapanda viwango vya Afrika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment