04 May 2012

DC awashauri waandishi kuzitumia kalamu vema



Na Theonestina Juma, Kagera

WAANDISHI wa habari mkoani Kagera wametakiwa kuwa makini katika kuelimisha jamii juu ya rushwa kutokana vitendo hivyo huathiri zaidi wananchi maskini kwa kushindwa kupata haki zao.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Bw. Samuel Kamote wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya waandishi wa habari wanachama wa Kagera Press Club (KPC) wapatao 34 yaliyodhaminiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) yanayofanyika mjini Bukoba.


Alisema, kutokana na vitendo vya rushwa kuathiri zaidi wananchi maskini kwa kuwakosesha kupata haki zao, hivyo waandishi wa habari wanalo jukumu na nafasi kubwa ya kuelimisha wananchi kuhusu wajibu na namna ya kuepuka rushwa.

Alisema, jamii inategemea waandishi wa habari kupitia vyombo vyao vya habari kupata ufafanuzi mbalimbali wa rushwa na hivyo wanatakiwa kuwa makini wanapoandika masuala ya rushwa ambayo yasipoandikwa na kutangawa kwa usahihi, yanawachang’anya wananchi.

Aidha, Bw. Kamote aliwataka waandishi hao kuwa waadilifu na waaminifu pindi wanapoandika habari zao kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao.

Pia aliwasihi wanahabari hao kutoingilia kesi ambazo zinachunguzwa na TAKUKURU kwa vile kufanya hivyo huathiri mwenendo mzima wa uchunguzi wao.

Alisema, waandishi hao wanatakiwa kujielimisha zaidi na kufahamu vizuri sheria za kupambana na kuzuia rushwa ya mwaka 2007.

Aidha, kwa upande wa Kamanda wa TAKUKURU mkoani Kagera Bi. Domina Mukama alisema lengo la mafunzo hayo ni kukuza uelewa kwa waandishi wa habari juu ya rushwa ili kuweza kufahamisha umma juu ya suala hilo.

Alisema, mafunzo hayo ni mwendelezo wa mipango ya TAKUKURU katika kushirikiana na vyombo vya habari ili kuwawezesha waandishi wa habari kuandika kwa usahihi taarifa zinazohusu rushwa.

No comments:

Post a Comment