29 May 2012

Ash aivaa Serikali mauaji ya albino


Na David John, Aliyekuwa Shinyanga

SERIKALI imeshauriwa kuwasaidia waandishi wa habari ambao wanaripoti habari za mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na siyo kuwawekea vikwazo vya kuwatisha pindi wanaporipoti habari hizo.

Mwito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Under The Same Sun Bw. Peter Ash mkoani Shinyanga baada ya kutembelea Shule ya Msingi Buhangija ambayo imefanywa kuwa moja ya kituo cha kulelea watoto wenye ulamavu wa ngozi.


Kituo hicho kilitengwa na Serikali baada ya kutokea mauaji ya albino miaka sita iliyopita.

Bw. Ash alisema kuwa anatambua kuwa serikali itakuwa inajisikia vibaya hasa kuendelea kuripotiwa kwa habari hizo kwa kutambua kuwa mauaji hayo yametia doa utulivu na amani ya nchi katika nyanja za kitaifa na kimataifa.

"Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikisomeka kuwa ni miongoni mwa nchi ambayo imefanikiwa kulinda amani na utulivu wa nchi, lakini baada ya kutokea mauaji hayo yamechafua uhalisia wa amani ya nchi,"alisema Bw Ash.

Alisema ili serikali ionekane haiungi mkono mauaji ya walemavu wa ngozi inatakiwa kuendelea kuunga mkono waandishi wa habari kupinga mauaji hayo ili kulisafisha taifa liendelee kuonekana kuwa ni kisiwa cha amani na upendo.

Mbali na rai hiyo Bw. Ash alitumia fursa hiyo kutoa vifaa mbalimbali kwa watoto hao ikiwa pamoja na miwani kwa ajili ya kujikinga na jua, kofia, madawa ya ngozi, losheni za kujipaka kwa ajili ya kuzuia miozi ya jua.

No comments:

Post a Comment