05 April 2012

Mzimu wa Arumeru wamgeukia Mrema

Na Bahati Mohamed
WANACHAMA wa Chama cha Tanzanian Labour Party (TLP), wamempa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Bw. Augustino Mrema muda wa siku 40 awe amejiuzulu wadhifa wake kwa madai ya kuchangia chama hicho kishindwe katika uchaguzi wa mdogo wa ubunge Jimbo Arumeru Mashariki, mkoani Arusha.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Hamad Tao, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema tamko la kumtaka Bw. Mrema kujiuzulu analitoa kwa niaba ya wanachama wa chama hicho kutokana na matokeo mabaya ya kura 18 walizopata katika kata zote za jimbo hilo na kusisitiza kama atashindwa kujiuzulu ndani ya muda huo, wataitisha  maandamano nchi nzima ili kushinikiza aondoke.

“Bw. Mrema alipewa fedha za kutosha kwa ajili ya kampeni lakini hatukuona alichofanya zaidi ya kuzitumia kwa matumizi binafsi,” alisema Bw. Tao.

Aliongeza kuwa, wanachama wa TLP hawakuridhishwa na uchaguzi uliofanyika katika chama chao juu kumpata mtu ambaye atawania nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki.

Alisema aliyechaguliwa kugombea nafasi hiyo kwa tiketi ya TLP si mwanachama wa muda mrefu bali alipewa kadi ya uanachama akitokea CCM ili aweze kuwania nafasi hiyo.

Bw. Tao aliipongeza CHADEMA kwa kupata ushindi katika uchaguzi uliofanyika Arumeru Mashariki.

No comments:

Post a Comment