Na Amina Athumani
TIMU ya taifa ya soka ya wanawake (Twiga Stars), imepewa msaada wa jezi na Kampuni ya Galileo by Travelport kwa ajili ya kuisaidia katika maandalizi yake ya kukata tiketi ya kucheza Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC), zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi msaada huo, Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Margret Leslie alisema ingawa msaada wao ni mdogo lakini wamejikuna walipoweza ili kuhakikisha nao wanatoa msaada wao kwa timu hiyo.
"Tunatoa jezi, maji na soksi kwa timu hii ya wanawake kama sehemu ya msaada wetu, tunaamini msaada huu utawasaidia wachezaji hawa katika mazoezi," alisema Margret.
Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura aliishukuru kambpuni hiyo kwa msaada huo ambao alisema kwao TFF ni mkubwa kwa kuwa timu hiyo haina mfadhili.
Twiga Stars ambayo iko kambini mkoani Pwani tangu Machi 25 mwaka huu chini ya Kocha Boniface Mkwasa, inajiwinda kwa fainali hizo mechi ya kwanza itacheza Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa, dhidi ya Ethiopia.
No comments:
Post a Comment