04 April 2012

Haroun Mahundi; IGP wa mwisho wa Nyerere aliyetuachia mafunzo mengi

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kiwete akimpa pole IGP wa zamani, Bw. Haroun Mahundi alipofiwa na mkewe, Bi. Clara Francis Mahundi mwaka 2010.


Na Masoud Sanani
MOJA ya mambo ambayo yananisumbua na kunipa taabu kubwa ni kuandika tanzia. Suala hili kwangu naliona gumu kwani huniongezea majonzi ya msiba husika.

Kwa kweli nimeshindwa pamoja na ugumu huu nimelazimika kuandika tanzia juu ya kifo cha aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania, IGP Haroun Guido Mahundi.

Licha ya uzoefu wangu wa miaka mingi katika tasinia ya uandishi wa habari na katika miaka hiyo nimeguswa na vifo vingi lakini nimeandika tanzia ambazo zinaweza kuhesabika.

Nakuwa mzito na hata ninapojaribu kuandika huwa nashindwa nikifika katikati na huwa naachia na kwa hiyo hakuna anayejua kama kulikuwa na tanzia inayoandikwa juu ya kifo fulani.

Inakuwa siri yangu na kwa kweli pamoja na kuniumiza roho kwa kutoandika tanzia kwa mtu ambaye nilikuwa namthamini naugulia moyoni na mambo yanapita.

Lakini, leo nimeshindwa kujizuia kutoandika angalau kidogo juu ya mzee Mahundi. Namuomba Mwenyezi Mungu anipe nguvu ili niweze kuandika aya chache juu ya muungwana huyu aliyetutoka juzi Jumatatu, Aprili 2, 2012 na kuipa kisogo dunia.

Ya kwake yamekwisha katika dunia hii. Ametuachia sisi tuliobaki mzigo wa dunia huku tukiwa hatujui nani atafuata baada ya yeye.

IGP Mahundi kama wengi tulivyozoweya kumwita alikuwa mmoja wa watu wenye mioyo thabiti na wenye ujasiri wa hali ya juu. Hakukuwa na jambo linalomtetemesha na kama lilikuwepo basi hiyo ilikuwa siri yake kubwa, kamwe usingeweza kumuona kahamanika na kakosa raha kwa jambo fulani.

Mara zote alikuwa mtu shujaa ambaye alikuwa analikabili lolote lililo mbele yake kwa ujasiri wa hali ya juu na kulitafutia jawabu la uhakika.

Hakuwa mcheshi kwa maana ya kucheka ovyo ovyo bali katika maisha yake mara nyingi tabasamu lilikuwa ndilo pambo la haiba yake.

Tangulia Mahundi, nyuma yako tunakufuata. Kwa kweli una hazina kubwa ya kijifunza kutoka kwako tangu uadilifu kazini na hata katika njia za kuhangaika kutafuta riziki ya kila siku.

Licha ya Mahundi kufika cheo kikubwa na cha mwisho katika kazi yake aliyoipenda ya polisi kwa kuwa IGP, alipostaafu mwaka 1995 baada ya Uchaguzi Mkuu hakusita kurudia taaluma yake ya sheria ambayo aliisomea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa kazini.

Hili la kuwa kazini na kusoma ni funzo kubwa kwa watu wengi kuwa elimu haina mwisho na siku zote mtu ana nafasi ya kujiendeleza kimasomo kama alivyofanya marehemu Mahundi. Alipata shahada yake ya Sheria mwaka 1978.

IGP Mahundi aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wa mwisho wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye sasa naye ni marehemu atakumbukwa zaidi kutokana na utumishi wake uliotukuka.

Mzee Mahundi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwalimu Nyerere mwaka 1984 wakati huo akiwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Arusha (RPC).

Akaitumikia nafasi hiyo hadi kung'atuka kwa Mwalimu Nyerere mwaka 1985 na kuendelea kuwa katika wadhifa huo kwa vipindi vyote viwili vya utawala wa Rais wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi hadi mwaka 1995. Rais wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa alimteua IGP Omar Mahita kushika wadhifa huo.

Mwanasheria Mahundi katika uhai wake aliliongoza Jeshi la Polisi na ikawa moja ya tasisi za serikali nchini ambayo ina uwazi na uwajibikaji.

Afande Mahundi alikuwa mtu wa watu. Hakuwa mbaguzi wa kuchagua kuzungumza naye kila mmoja alimpa nafasi na kusikiliza mawazo yake na kama kuna kitu cha kuchukua na kukifanyia kazi hakusita kufanya hivyo.

Marehemu ametuachia kuwa hakuna kitu muhimu zaidi duniani kama kazi. Alikuwa mtendaji mzuri ambaye amefanya kazi zake hadi mwisho wa uhai wake.

Alistaafu kazi ya kuajiriwa na serikali, lakini hakustaafu kufanya kazi. Hilo ni jambo jema ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujifunza kutoka kwake.

Mahundi akiwa na miaka 72 bado alikuwa akichapa kazi kila siku. Alikuwa anafanya shughuli nyingi kuliko baadhi ya vijana, kitu ambacho licha ya maumivu ya maradhi yaliyokuwa yakimkabili bado hakuwa mtu wa kutulia.

Kama asilimia kubwa ya Watanzania wangeiga mfano wa kufanya kazi wa marehemu Mahundi nchi hii itatoka katika umasikini ilionao na kuwa moja ya nchi zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo.

Kwa kweli hakuna maneno ya kutosha ya kuweza kumsifu Mahundi itoshe tu kwa kusema kwamba ametuachia mengi ya kujifunza na mengi ya kumuiga kama mwanadamu anataka kupata mafanikio.

Mahundi aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Polisi wa Kimataifa (Interpol) katika uhai wake. Pia Februari 2003 Mahundi alijiunga na FK Law Chambers akiwa mshirika mkuu.

Mbali na kazi zingine kadhaa mabazo alizifanya katika uhai wake pia alikuwa mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), mjumbe wa Bodi ya Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA), wakili wa Mahakama Kuu Tanzania na mjumbe wa bodi wa mashirika mbalimbali.

Alikuwa mwanachama wa Chama cha wanasheria wa Tanganyika, Afrika Mashariki na jumuiya zingine.

Marehemu Mahundi aliyefiwa na mkewe, Clara Francis Mahundi Machi 12, 2010 ameacha watoto wanne, Francis,Grace, Flora na John na anatarajiwa kuzikwa Jumamosi kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam kwa mapumziko ya milele. Marehemu Mahundi atazikwa jirani na kaburi la mkewe.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amina.

1 comment: