16 April 2012

Shule za msingi, sekondari zakabiliwa tatizo la mimba

Na Pendo Mtibuche, Dodoma
HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma, bado inakabiliwa na tatizo la mimba katika shule mbalimbali za msingi na sekondari.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Bi. Betty Mkwasa, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wadau wa elimu na kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi.

Alisema tatizo la mimba na utoro kwa wanafunzi limekuwa sugu na kuwaomba wadau hao, waone umuhimu wa kulitafutia ufumbuzi.

Bi. Mkwasa alisema tatizo hilo linatokana na changamoto mbalimbali za baadhi ya wanafunzi wa sekondari kutembea umbali mrefu, kukosekana kwa hosteli na zile zilizopo nyingi hazitambuliki 'bubu' na hazina ulinzi kwa watoto hao.

Aliongeza kuwa, wanafunzi wengi wa kike wanaosoma sekondari wamepanga mitaani ambapo nyumba wanazoishi si salama kwa maisha yao jambo linalosababisha baadhi ya wasichana kuingia kirahisi katika vishawishi.

“Halmashauri hii pia inakabiliwa na tatizo kubwa la utoro kwa wanafunzi shuleni hivyo kusababisha wale wanaofaulu shule ya msingi kwenda sekondari, kutoripoti shuleni na hawafuatiliwi.

“Kutokana na hali hii, nawaagiza Watendaji wa Kata na Vijiji, kuhakikisha mnawafuatilia wanafunzi watoro na kuwachukulia hatua wazazi au walezi wa wao,” alisema Bi. Mkwasa na kusisitiza kuwa, suala la miundombinu katika shule mbalimbali za msingi na sekondari hairidhishi.

Alisema halmashauri hiyo inakabiliwa na upungufu wa nyumba za walimu, matundu ya vyoo kwa shule mbalimbali na thamani za shule hivyo aliwaomba wadau hao kutafuta ufumbuzi.

No comments:

Post a Comment