Na Pendo Mtibuche, Dodoma
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw.Samuel Sitta, amesema umefika wakati wa Serikali kufanya kazi kwa uwazi katika mambo mbalimbali.
Bw.Sitta aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la nyongeza ambalo liliulizwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw.Zitto Kabwe (CHADEMA).
Katika swali hilo, Bw.Kabwe alitaka kujua kwanini Serikali inaendelea kuiacha Kampuni ya simu za mkononi (TIGO), iendelee kujiendesha kwa asilimia 100 bila ubia wa wazawa kama zinavyofanya kampuni nyingine za simu nchini.
Bw.Kabwe alisema, mwaka 2005 kampuni hiyo ilikuwa na hisa lakini baada ya Uchaguzi Mkuu kumalizika na rais kuapishwa, hisa za kampuni hiyo ziliuzwa kinyemela hivyo kwanini Serikali inaendelea kuiacha ikifanya kazi bila kufuata sheria.
Ufafanuzi wa Bw.Sitta kuhusu swali hilo, ulitokana na majibu yake yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw.Charles Kitwanga, kutojitosheleza.
Hata hivyo, wakati Bw.Kitwanga akijibu swali hilo alimtaka Bw.Kabwe akasome sheria na kanuni za uanzishwaji kampuni za simu kwa madai kuwa, pengine haifahamu vizuri.
Baada ya majibu hayo, Bw.Sitta ambaye kwa sasa ni Kaimu Kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, alilazimika kusimama na kutoa ufafanuzi wa jambo hilo.
“Ukilitazama suala hili, ndani yake yawezekana lina umuhimu hivyo kama Serikali lazima tufanye kazi kwa uwazi, tukae na kuangalia jambo hili upya ili tuone majibu yake yanakuwaje,” alisema.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Mpanda Mjini, Bw.Said Arfi (CHADEMA), alitaka kujua kwanini hisa za Kampuni ya simu za mkononi ya Zain, hazikupelekwa katika Soko la Hisa jijini Dar es Salaam na kuuzwa kwa Watanzania badala yake zikauzwa kwa Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kinyume na sheria inayotaka hisa hizo ziuzwe kupitia soko la hisa.
Akijibu swali hilo, Bw.Kitwanga alisema hivi sasa Serikali ina hisa asilimia 40 katika Kampuni ya Airtel ambayo awali iliitwa Zain Tanzania na Kampuni ya Celtel Tanzania BV, inamiliki asilimia 60 ya hisa.
Aliongeza kuwa, wakati wa Serikali kuuza hisa ukifika, utaratibu utawekwa kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kutoa fursa kwa Watanzania kununua hisa.
No comments:
Post a Comment