12 April 2012

Dhana ya kujitegemea itachochea maendeleo

WAKATI Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere anajenga misingi ya Taifa hili baada ya uhuru, alitangaza siasa ya ujamaa na kujitegemea.
Mwalimu Nyerere aliamini kuwa, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa kutegemea nguvu ya Watanzania badala ya kutegemea misaada kutoka nje.

Alihamasisha matumizi ya rasilimali za ndani ili kukuza uchumi wa nchi na kupinga kwa nguvu zote misaada kutoka nje akiamini kuwa, inadumaza maendeleo na fikra za Watanzania.

Chini ya mtazamo huo, miaka michache baada ya uhuru, Tanzania ilipiga hatua kubwa kimaendeleo na kuanzisha viwanda mbalimbali kikiwemo cha zana za kilimo.

Kutokana na msimamo wa Mwalimu, Tanzania ikawa juu kiuchumi miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki lakini hivi karibuni, viongozi wetu wameacha kuhamasisha moyo wa kujitegemea.

Sisi tunasema kuwa, dhana ya kujitegemea bado ina umuhimu mkubwa kwa Watanzania kama sera ya Ujamaa imepitwa na wakati.

Badala ya viongozi wetu kuhamasisha wananchi kujitegemea wamegeuka mabingwa wa kuhangaika kupita huku na kule kuomba misaada.

Jambo la kusikitisha, bingwa wa kuomba misaada na kupeleka kwa wananchi wake ndiye anaonekana kiongozi bora.

Mfano mzuri ni namna wabunge wanavyohangaika sasa kutafuta misaada ya kila aina ili waweze kuipeleka katika majimbo yao.

Kwa utamaduni uliozoeleka sasa, anayepeleka misaada jimboni ndiye anaonekana anafanya kazi nzuri na ana nafasi kubwa kuchaguliwa tena.

Ukweli ni kwamba, wajibu wa kiongozi hasa mbunge sio kuhangaika kutafuta misaada na kugeuka 'omba omba', tabia ambayo Mwalimu Nyerere aliikataa.

Umefika wakati wa wabunge kuhakikisha, wananchi wanajengewa moyo wa kujitegea ili kuharakisha maendeleo ya sekta mbalimbali.

Imani yetu ni kwamba, wajibu wa mbunge ni kuhamasisha, kuandaa na kusimamia wananchi wake kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali chache walizo nazo.

Kwa kufanya hivyo watasaidia kupatikana maendeleo endelevu yatakayosadia wananchi kukuza kipato chao na kubadilika kifikra.Tubadili mizamo.

No comments:

Post a Comment