16 April 2012

Balozi Mwapachu awapa somo vijana

Na Willbroad Mathias
ALIEKUWA Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu, amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo ya sekta mbalimbali nchini na kuwataka waache dhana ya kujiona wao ni viongozi wa kesho.

Balozi Mwapachu aliyasema hayo Dar es Salaam juzi, katika mkutano wa Mawasiliano wa Masoko (MCC) ulioandaliwa na kampuni ya MIL na kushirikisha wadau mbalimbali.

“Mimi naona vijana ni viongozi wa leo si kesho hivyo mnapaswa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi,” alisema Balozi Mwapachu na kuwataka viongozi wa Serikali kujenga utamaduni wa kukutana na vijana mara kwa mara ilikujadili matatizo mbalimbali yanayolikabili Taifa.

Awali katika mada yake ya kutangaza bidhaa ambazo zinazalishwa nchini ili kuteka masoko ya Kimataifa, Balozi Mwapachu aliwataka washiriki wa mkutano huo kufikiria jinsi ya kulitangaza Taifa kwa kutambulisha bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Tulijivunia mengi wakati wa utawala wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa sababu aliitangaza Tanzania hivyo kwa msingi huo ilisaidia bidhaa zetu kutambulika kwenye masoko ya kimataifa,” alisema Balozi Mwapachu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw. Rodgers Mbaga, umefika wakati wa Watanzania kupata mawazo mapya ya kupenyeza bidhaa katika masoko ya nje kutokana na uzoefu waliopatiwa kupitia mada mbalimbali zilizotolewa.

“Tunaelewa kuwa, zipo fursa mbalimbali za wadau wa masoko ambazo tukizifanyia kazi zinaweza kuleta mabadiliko na sisi tutaandaa semina nyingi kama hii,” alisema.

No comments:

Post a Comment