19 March 2012

Wanaotajwa kuwania UWT watuhumiwa kugawa rushwa

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAANDALIZI ya kuwania nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Chama Cha Mapinduzi (UWT) yameingia katika sura mpya baada ya wanachama wake kudaiwa kuanza kampeni kabla ya muda.

Wakati kampeni hizo za chini kwa chini zikiendelea baadhi ya watu ambao wanatajwa kuwania nafasi hiyo wametuhumiwa kugawa rushwa kwa wajumbe kama kishawishi cha kuweza kuchaguliwa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya UWT ambazo zinawahusisha baadhi ya wabunge akiwemo mmoja kutoka Mkoa wa Kilimanjaro (jina tunalo) zilidai kuwa wenyeviti wa wilaya na mikoa waliokuwa wakihudhuria semina elekezi kuelekea uchaguzi wa ndani ya CCM.

Sambamba na nafasi ya mwanamke katika kuwania uongozi iliyofanyika Machi 13-14, mwaka huu mjini Dodoma mbunge huyo aliweza kutumia nafasi hiyo kuwashawishi wampigie kura.

Katika semina hiyo, inadaiwa mbunge huyo (jina tunalo) alitumia nafasi hiyo hasa muda wa jioni na kufanya ushawishi kwa viongozi hao wa wanawake wa mikoa na kuwataka kumchagua yeye kwani Mwenyekiti wa sasa UWT (Sophia Simba) hatakiwi kwa wabunge wanawake wa CCM.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi viongozi hao wa mikoa wa UWT, walidai wakati wa semina hiyo elekezi mbunge huyo (jina tunalo) alitumia nafasi hiyo na kueleza dhamira yake huku akiwatadharisha hasa kwa wale waliopewa fedha Sh. 30,000 kwa kila mmoja kutambua umuhimu wa mchango huo katika kumchagua.

Hata hivyo kwa mujibu wa mmoja wa makatibu wa UWT mkoani Morogoro alimdokeza mwandishi wa habari hizi kuwa yeye ni mmoja wa watu waliofika katika kikao hicho kilichoitishwa na mbunge huyo na kupewa Sh. 30,000 kama ushawishi wa kumuunga mkono mgombea huyo.

“Katika kikao kile tulikusanywa usiku na kupelekwa katika Hoteli ya Fifty Six, iliyopo jirani ya jengo la Bunge na kupewa fedha, lakini baada ya kupokea alituambia hela...haiendi bure, na kama ukiichukua na ukienda kinyume utakufa, tena akisema atatulisha yamini wote aliotupa fedha.

“Alitumia nafasi hiyo hasa pale tulipokuwa katika semina ambapo wanawake wengi kutoka mikoa yote tulimsifu Sophia Simba, kuwa ana haki ya kugombea kutokana na ameisadia UWT vizuri na hata maslahi ya wanawake kuweza kudhaminiwa ndani ya chama chetu cha CCM. Kwani kauli hiyo ilimuuma na hata kuanza kutoa vitisho dhidi yetu," alidai mmoja wa Katibu huyo kutoka mkoani Morogoro.

Hata hivyo awali chanzo hicho kilidokeza kuwa mbunge huyo ambaye anaonesha ushawishi mkubwa wa kutaka kuwania nafasi hiyo aliwawakusanya wanawake hao kupitia kwa mmoja wa wanawake (jina tunalo) ambaye ni mmoja wa watumishi waandamizi wa CCM Makao Makuu Mjini Dodoma pamoja na viongozi wengine waandamizi kufanya vikao tofauti kwa ajili ya ushawishi.

Chanzo hicho kilidai kuwa viongozi wa UWT wa mikoa ambao walifanya vikao na Mbunge huyo ni pamoja na mkoa wa Shinyanga, Dodoma, Singida, Kilimanjaro, Kigoma na Morogoro, ambao kila mmoja alipewa posho ya sh. 30,000 ili kama njia ya kufanikisha harakati zake.

Katika vikao hivyo pia Mbunge huyo inadaiwa alitumia muda mwingi kujitabirisha kama mbunge mpambanaji katika rushwa huku akiungwa mkono na wabunge wote wa viti maalum kutoka CCM, ambapo alihidi pindi akiwa Mwenyekiti wa UWT ataondoa suala la kuwa na ukomo wa Ubunge wa Viti Maalum.

Hata hivyo jitihada za kupata ufafanuzi kwa mbunge huyo kwa njia ya simu ambaye anatuhumiwa kuwashawishi wanawake kumchagua ili kuwania nafasi hiyo kupitia uchaguzi wa Desemba mwaka huu alidai kuwa, hana vita wala chuki na mtu badala yake hao wanaosema wanambebesha mzigo ambao si wake kwani hata uchaguzi wa matawi haujafanyika na hawezi kufanya hivyo.

Katika hatua nyingine mara baada ya mwandishi wa habari hizi kuwasiliana kwa njia ya simu na kiongozi wa ngazi za juu kutoka CCM (jina tunalo) ili kupata ufafanuzi iwapo wanatambua mambo yote hayo yanayoendelea, alikiri kuwepo kwa udhaifu huo na akamuhakikisha mwandishi kuwa hilo ni tatizo la kimfumo na siku si nyingi chama kitaliondoa kabisa.

“Hivi sasa tuna tatizo la kimfumo na muda mwingi tumekuwa tukitumia busara katika kuyaendea haya, tunaangalia utaratibu mzuri ambao utatusaidia kuondoka huko," alidai kiongozi huyo.

No comments:

Post a Comment