Na Eliasa Ally, Njombe
WAZIRI wa Mali Asili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige amemtaka Meneja wa Mali Asili na Misitu wa Wilaya ya Njombe mkoani Njombe, Bw.Benson Kibonda kutolea taarifa sahihi za ujenzi wa nyumba mbili za kukaa maofisa na nyingine jengo la ofisi kutokana na kushindwa kukamilika.
Alisema ujenzi huo umeshindwa kukamilisha tangu mwaka 2004 hadi sasa jambo ambalo linaonesha kuna tatizo.
Bw.Maige alihaidi kutokana na hali hiyo atamtuma Mkaguzi wa ndani kutoka wizarani kutokana na kuwa kila mwaka nyumba hizo mbili zimekuwa zikiombewa bajeti na kutilia shaka kuwa hata mwaka huu ameshangazwa nyumba hizo kuombewa bajeti.
Akizungumza katika ofisi za wilaya hiyo mwishoni mwa wiki, Waziri Maige alisema, haridhishwi na ujenzi wa nyumba hizo ambazo zilianza kujengwa mwaka 2004 na hadi sasa ujenzi wake bado haujakamilika wakati pesa nyingi zimetumika.
Alisema, katika taarifa alizonazo zinaonesha kuwa mwaka 2004 nyumba hizo zilipoanzwa kujengwa Serikali chini ya wizara yake ilitoa pesa ambapo katika kujenga nyumba ya kukaa watumishi zilitolewa sh.milioni 61 huku ujenzi wa ofisi ya Mali Asili zikitolewa sh. milioni 26 lakini hadi sasa ujenzi unasuasua.
"Hatua zitachukuliwa za kujirithisha na matumizi ya pesa ambazo zinatolewa serikalini kwa kuwa ujenzi huu umeanza toka mwaka 2004, baada ya kutolewa pesa hizo, lakini hadi sasa tunaoneshwa majengo ambayo hayajakamilika nitahakikisha Mkaguzi wa ndani kutoka wizarani anatumwa kufanya uchunguzi wa pesa zote zilizotumiwa ili tuwe na majibu kamili,"alisema Bw. Maige.
Akizungumzia ujenzi wa nyumba za kukaa watumishi wa Mali Asili na ofisi zilizokuwa zinajengwa, Meneja Miradi wa Ujenzi wa Nyumba za Mali Asili, Bw. Benson Kibonda alisema, yeye kwa sasa hana taarifa yoyote kuhusiana na matumizi ya pesa ambazo zilitolewa na serikali ili kugharimia ujenzi wa nyumba hizo.
"Zaidi ya mameneja watatu wamepita wakati wa ujenzi wa nyumba hizi, mimi mwenyewe niliyepo kwa sasa sina hata taarifa sahihi kuhusiana na ujenzi wa nyumba hizi...na sielewi chochote, siwezi kutolea taarifa za uongo kwa sasa," alisema Bw. Kibonda.
Aidha, aliongeza katika ujenzi wa nyumba za kukaa watumishi wa mali asili na ofisi katika eneo la Kipengele Njombe kulikuwa na lengo la kutaka kutatua watumishi hao kuendelea kukaa mbali ambapo walikuwa wanatumia nyumba zilizopo Ilembula sehemu ambayo ilikuwa na ofisi za muda.
No comments:
Post a Comment