20 March 2012

Ngawaiya akemea kauli za kejeli kwa Mzee Mkapa

Na Peter Mwenda
JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Kilimanjaro, imelaani kauli za kejeli dhidi ya viongozi wastaafu zinazotolewa kwenye kampeni zinazoendelea katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Bw. Thomas Ngawaiya, alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Majira.

Alisema kauli za kejeli zinazotolewa na vyama pinzani vya siasa dhidi ya Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa ni utovu wa nidhamu.

“Tunalaani matusi na kashfa zilizotolewa kwa rais mstaafu kwani ni kinyume cha mila na desturi zetu za Kitanzania, kijana kumtusi Mzee ambaye ni sawa na baba yake mzazi ni utovu mkubwa wa nidhamu,” alisema Bw. Ngawaiya.

Alisema jumuiya hiyo inapenda kuona wanasiasa wanashindana kwa hoja si matusi au kukashfiana jukwaani na kuongeza kuwa, kama Bw. Mkapa alikosea kwenye hotuba yake, hakukuwa na sababu ya Mbunge wa Musoma Mjini, mkoani Mara kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Vincent Nyerere, angemkosoa taratibu badala ya kumkashifu.



Aliongeza kuwa, jumuiya hiyo inaamini Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kama angekuwa hai, angemwadabisha Bw. Nyerere kwa kumuita Bw. Mkapa muasisi wa ufisadi.

“Bw. Mkapa alipokuwa madarakani, alifanya kazi kubwa ya kujenga uchumi wa nchi uliokuwa umeharibika na anasifiwa duniani kote, bila mchango wake demokrasia ya vyama vingi isingefika hapa ilipo,” alisema Bw. Ngawaiya.

Alisema Serikali ya Mkapa ilimuuguza Mwalimu Nyerere wakati anaumwa na baada ya kufariki alizikwa kwa heshima zote.


1 comment:

  1. Tatizo kubwa CCM mnaangalia upande mmoja wa shilingi. Angetamka mtu wa CHADEMA yale aliyotamka Mkapa ingekuwa Nongwa. Inakuwaje Rais mstaafu badala ya kunadi sera na kumtambulisha mgombea wako unaanza kumsema mtu binafsi? Pale hawaendi kutafuta mchumba bali mwakilishi wa wananchi. Kilichotakiwa ni kumwaga sere na sio vinginevyo. Mkapa alikosea. Akubali yaishe.

    ReplyDelete