20 March 2012

Dkt. Slaa azidi kutema cheche Arumeru

*Akemea CCM kugeuza kifo cha Sumari 'mtaji'
Na Mwandishi  Wetu, Arumeru
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willbroad Slaa, amewataka wakazi wa Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, kupuuza ahadi zinazotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni humo ili wamchague mgombea wao Bw. Sioi Sumari.

Dkt. Slaa aliyasema hayo jana wakati akimnadi mgombea wa chama hicho Bw. Joshua Nassari, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye eneo la Kikwe Nambala.

Alisema ahadi zinazotolewa na CCM hazitekelezeki na kusisitiza kuwa, kauli iliyotolewa na Mbunge wa Mtera, mkoani Dodoma Bw. Livingstone Lusinde kuwa Bw. Sumari anastahili kupewa ubunge ili kumpoza kutokana na kifo cha baba yake mzazi haina mashiko.

“Kauli hii inadhihirisha wazi kuwa ndani ya CCM kuna utawala wa kichifu, chama hiki kinapaswa kunadi sera zao kwa wananchi si vinginevyo, wasitumie kifo cha Bw. Jeremiah Sumari kama mtaji.

“Mzee Sumari tumemzika hivi karibuni, hata kaburi lake halijaota majani, leo hii CCM wanasema mtoto wake apewe ubunge ili kumuondolea machungu, wakazi wengi waishio hapa Arumeru Mashariki wameondokewa na wazazi wao, sasa nani wa kuwafuta machozi kama sio kuwanyima haki zao,” alihoji Dkt. Slaa.


Katika hatua nyingine, Dkt. Slaa alisema chama chochote ambacho kinaonekana kufanya kampeni kwa mbwembwe huku wakionekana kujitenga, kuwa hawajiamini na wanachofanya hivyo wapiga kura wanapaswa kukiangalia vizuri.

Alisema chama cha siasa kinapaswa kuwaeleza wananchi jinsi watakavyoweza kuwasaidia wananchi si kutoa maneno ya kashfa ambayo yanalenga kuleta mtafaruku ndani ya jamii.

“Kampeni si mbwembwe bali ni njia ya kuielezea jamii jinsi utakavyoweza kuwasaidia,” alisema.

Kwa upande wake, Bw. Nassari alisema wananchi wanatakiwa kuachana na aina zote za propaganda na kuangalia kiongozi ambaye atawasaidia bila kujali itikadi zao kisiasa. 

No comments:

Post a Comment