20 March 2012

Lowassa aliangukia Kanisa Katoliki

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu aliyejiuzuli, Bw. Edward Lowassa, amelitaka Kanisa Katoliki kuisaidia Serikali kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.
Bw. Lowassa aliyasema hayo juzi wakati akitoa salamu katika hafla ya uzinduzi wa Jimbo Jipya la Kanisa Katoliki Ifakara, mkoani Morogoro ambao ulikwenda sambamba na kusimikwa kwa Askofu mpya wa jimbo hilo, Salutaris Libena.

“Nawaomba Maaskofu, katika miradi yenu mlipe kipaumbele suala ajira kwa vijana, wengi wao wanamaliza elimu ya sekondari na vyuo lakini hawana ajira, hili ni bomu linalosubiri kulipuka.

“Kutokana na hali ilivyo, naliomba kanisa lisaidie juhudi za Serikali kutatua tatizo hili, hali ngumu ya maisha iko kote duniani, mataifa makubwa nayo yanamaatatizo lakini mataifa madogo kama Tanzania, hali inakuwa mbaya zaidi,” alisema Bw. Lowassa.

Aliwaomba Maaskofu kuwaombea viongozi wa nchi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, bidii, haki na kumtegemea Mungu.

Katika salamu zake, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alimtaka Askofu Libena kutumia nafasi yake kuleta amani na upendo kwa Watanzania.

Akizungumza katika sherehe hizo, Rais wa Baraza Maaskofu Tanzania, Askofu Yuda Dadeus Ruaichi, alisema mgomo wa madaktari umeiletea aibu Tanzania.

“Watanzania wengi wamepoteza maisha kwa kukosa matibabu kutokana na mgomo, hii imeonesha Taifa la Tanzania halina dira, hakuna uharaka uliochukuliwa kushughulikia mgomo ule.

“Kimsingi nchi yetu imefikia kubaya kwa kuonekana imeshindwa kushughulikia matatizo,” alisema.

Katika salamu zake, Askofu Libena alisema kanisa hilo litaendelea kupambana na umaskini uliopo kwenye jamii.


No comments:

Post a Comment