20 March 2012

Mwakyembe arejea kazini, aitega polisi

*Akataa kuzungumzia ugonjwa wake, asema yuko 'fiti'
*Amshukuru Rais Kikwete, wapiga kura, Watanzania


Naibu Waziri wa Ujenzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam jana, baada ya kuingia ofisini kwake kwa mara ya kwanza na kuanza kazi rasmi, baada ya kuugua, ikiwa pamoja na kuwatoa wasiwasi wananchi kuwa amepona na kuanza kazi. (Picha na Peter Mwenda)

Na Peter Mwenda
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, amesema baada ya kurejea nchini akitokea India ambako alikuwa akipatiwa matibabu, hivi sasa yupo 'fiti' kiafya hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi wowote.

Dkt. Mwakyembe aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ikiwa ni mara yake ya kwanza kuripoti kazini baada ya kutoka kwenye mabitabu.

Alisema hivi sasa ni mzima kabisa ila hawezi kuzungumza lolote kuhusu chanzo cha ugonjwa uliokuwa ukimsumbua kwani suala hilo ameliacha serikalini ili waweze kufanya uchunguzi wa kina.

“Nipo tayari kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kama watakuja kunihoji kuhusu chanzo cha ugonjwa uliokuwa ukinisumbua ambao unafahamika.

“Taarifa zaidi zitatolewa na Jeshi la Polisi baada ya kunihoji, natumia nafasi hii kuwaeleza wananchi kuwa, nilikuwa naumwa na sasa nimepona, afya yangu ipo salama kabisa, nina mafaili lundo yananisubiri, namshukuru Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli kwa kuendesha Wizara peke yake.

“Mwisho nawashukuru Watanzania wote kwa kuniombea sana na Rais Jakaya Kikwete ambaye amenitembelea nyumbani kwangu na kuhakikisha napata tiba iliyonifanya nifikia hali hii,” alisema.

Dkt. Mwakyembe pia alitumia fursa hiyo kuwalaumu waandishi wa habari kwa kuandika habari za ugonjwa wake kibiashara zaidi na kuweka vichwa vya habari vilivyoonesha yeye si mtu wa kupona.

Alisema hali hiyo iliitisha familia yake ambayo ilionekana kukata tamaa kama atapona na kusisitiza yupo hai na ataendelea kuwa hai.

Aliwashukuru wapiga kura wa jimbo la Kyela, mkoani Mbeya kwa kumuombea na kuahidi kwenda kuzungumza nao.

“Ugonjwa uliokuwa unanisumbua ni vigumu kuueleza, hata kwenye kamusi huwezi kujua ni ugonjwa gani ila badaktari pekee ndio wanaojua,” alisema.

Dkt. Mwakyembe aliwasili ofisini kwake saa 3:40 asubuhi na baadae kuzungumza na waandishi wa habari katika chumba cha mikutano.

Alianza kuugua 2011 na kupelekwa nchini India kwenye Hospitali ya Appolo kwa matibabu. Baada ya kupatiwa matibabu alirejea nchini na kurudi India kucheki afya yake.

Rafiki wa karibu na Dkt. Mwakyembe ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta, alidai ugonjwa unaomsumbua Dkt. Mwakyembe, ulitokana na kulishwa sumu.

Kauli hiyo ilikanushwa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, DCI Robert Manumba, ambaye alisema uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo unaonesha Dkt. Mwakyembe hakulishwa sumu.

Bw. Manumba alikanusha madai hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, wakati Bw. Sitta akititoa madai hayo jeshi hilo lilikuwa likifanya uchunguzi wa madai ya Dkt. Mwenyembe ya kutishiwa maisha kwa ujumbe mfupi wa simu yake.

Alisema kabla Dkt. Mwakyembe hajaugua na kupelekwa nchini India, alihojiwa kuhusu madai ya kutishiwa maisha.

“Tuliwasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi na Jamii kuhusu madai ya Bw. Sitta kuwa Dkt. Mwakyembe amelishwa sumu lakini tuliambiwa ugonjwa unaomsumbua hautokani na kulishwa sumu.

Bw. Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM) na Dkt. Mwakyembe, wote ni wapambanaji wakubwa katika vita dhidi ya ufisadi nchini.


           
   

No comments:

Post a Comment