21 March 2012

Simba yaingiwa hofu Bamba Beach

*Jabu nje wiki mbili
Na Zahoro Mlanzi
HOFU, hujuma zaanza kutanda! ndivyo utakavyoweza kusema baada ya vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba safari hii kukataa kuweka kambi Bamba Beach nje kidogo ya Dar es Salaam, kujiandaa na Kombe la Shirikisho dhidi ya ES Setif ya Algeria.

Simba itashuka uwanjani Jumapili kuumana na timu hiyo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni mechi ya pili ya hatua ya awali ya kombe hilo. Simba iliitoa Kiyovu ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana Dar es Salaam jana, zilieleza kwamba timu hiyo inahofia kupiga kambi Bamba Beach kutokana na mazingira ya hivi sasa kutokuwa mazuri kwa wachezaji wao.

"Juzi (Jumatatu) wachezaji walipewa mapumziko na jana asubuhi, waliendelea na mazoezi kama kawaida kwa kufanya ya gmy na baada ya hapo walikwenda kumpa pole mchezaji mwenzao, Rajabu Isihaka aliyefiwa na baba yake mzazi," zilieleza taarifa hizo.

Taarifa hizo zilieleza zaidi kwamba baada ya kutoa pole, kikosi cha timu hiyo kitaingia kambini rasmi kati ya hoteli za Girrafe iliyopo nje jiji la Dar es Salaam au Wanyama iliyopo Sinza, lengo kubwa kuwaweka wachezaji hao katika hoteli yenye hadhi.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage kuzungumzia suala hilo, alisema mpaka jana mchana hawakujua kama timu hiyo itaendelea kuweka kambi huko, au kuhama kwani taratibu zilikuwa zikiendelea.

"Awali tulikubaliana timu iendelee kuweka kambi Bamba Beach, lakini tangu juzi tumekuwa tukipeana taarifa tofauti tofauti juu ya kambi ila kila kitu kitakuwa wazi muda si mrefu," alisema Rage kwa njia ya simu.

Katika hatua nyingine, Daktari wa timu hiyo, Cosmas Kapinga alielezea hali za majeruhi mabeki Juma Jabu na Amir Maftah, ambapo alisema Maftah ameshapona lakini Jabu bado ni mgonjwa.

"Maftah amepona kabisa na atajiunga na wenzake mazoezini kesho (leo) asubuhi na Jabu, yeye bado anasumbuliwa na mamumivu ya kifundo cha mguu wa kushoto, ambapo atakuwa nje kwa wiki mbili," alisema Kapinga.




No comments:

Post a Comment