20 March 2012

Matumizi ya simu kwa wanafunzi yazuiwe

Na Anneth Kagenda
SERIKALI imeshauriwa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi shuleni kwa kuwa zinachangia wengi wao kufanya vibaya kwenye mitihani yao.
Ushauri huo umetolewa Dar es Salaam juzi na Diwani Viti Maalum Bi. Aisha Sululu, wakati wa kongamano la wanafunzi wa Dar es Salaam lililohusu chanzo cha wanafunzi kufeli mitihani yao.

"Kila kukicha nawaza nini kifanyike ili kuongeza ufaulu wa watoto wetu, kwani hali ni mbaya na huko tunakoelekea si pazuri hata kidogo," alisema Bi. Sululu.

Kwa mtazamo wake alisema anaona simu zikizuiwa mashuleni,hatua hiyo inaweza kuleta mabadiliko wakati mwingine mwalimu anakuwa anafundisha huku wanafunzi wakitumiana ujumbe na watu wengine na si kuangalia ubaoni.

"Na unapokuja hakuna anachokijua tumechoka kupata aibu kila siku na hawa walio unganisha mitandao ya ngono kwenye komputa wafungiwe haraka, kwani mtoto badala ya kusoma anaanza kuangalia ngono na mambo mengine ambayo hayana faida kwenye maisha yake," alisema Bi. Sululu.

Kwa upande wake Shekhe Mohamed Issa, alisema inafahamika wazi kwamba Watanzania hawana desturi ya kujisomea na kusema kuwa desturi hiyo inazidi kuathiri kizazi kizazi kutokana na kwamba ufaulu wa wanafunzi unapungua kila siku huku sababu nyingine ikiwa ni kuongezeka kwa utandawazi ambao nao umeathiri zaidi.

Alisema tofauti na hilo pia malezi kwa wazazi na wanafunzi yamepungua kwani  siku hizi watoto wa kiume haoni aibu kuvaa heleni, kusuka nywele kuvaa mavazi mengine ambayo si mazuri.


Aliwataka wanafunzi kuepuka  mambo yote yanayowafanya washindwe mitihani na kuwataka kuheshimu walimu na wazazi.

"Kwa upande wa wasichana kama kuna mwanaume anakusumbua toa taarifa kwa mwalimu au mzazi usibebe jambo peke yako na huo ndio ujasiri mnaotakiwa kuwa nao," alisema.

 

No comments:

Post a Comment