20 March 2012

Wajasiliamali wapewe mafunzo kukuza kipato

KUJIAJIRI ni suala linalopewa kipaumbele na mamlaka mbalimbali hapa nchini hata ngazi ya kimataifa
Kutokana na mabadiliko makubwa ya mifumo ya uchumi yanaendelea kutokea katika maeneo mengi hapa nchini na duniani kwa ujumla, yamechangia ajira nyingi kufungwa huku mamlaka na serikali husika zikipigia debe sekta binafsi na ajira binafsi.
Hapa nchini, hivi sasa watu wengi wameamua kujiajiri wenyewe wakiwemo wastaafu kwa kufungua vitega uchumi vyao zikiwemo biashara ndogo ndogo kwa lengo la kuwapatia mkate wao wa kila siku.

Kujiajiri hususani katika biashara ndogo ni jambo jema lakini sisi tunaona bado kuna  tatizo moja kubwa ambalo liwasibu wadau wengi walioangukia kwenye shughuli hizo nalo ni kukosa mafunzo ya namna ya kuendesha biashara na kukuza mitaji yao.

Wafanyabiashara ndogo wengi nchini hawabadiliki kutokana na kufanya shughuli zao kwa mazoea bila kuwa na ujuzi wa namna ya kuendesha biashara hizo.

Watu wengi waliostaafu wakapewa viinua mgongo vyao na kuwekeza kwenye biashara hizi, wamejikuta wakikabiliwa na wakati mgumu kwa kutafuna mitaji yao au kuwa na biashara zilizodumaa kutokana na mitaji hiyo kutokua.

Wenye biashara ndogo wakiwemo akina mama wauza maandazi na vitumbua wanafanya shughuli hiyo bila kuwa na mtazamo wa kutunza ziada wanazopata kwa kufungua akaunti, wanachoapata kinakwenda tumboni bila kujua kuwa hata senti 50 inayobaki, inastahili kuwekwa kama akiba kwa ajili ya mwendelezo wa biashara zao.

Hali hii ni ya hatari kwani kundi hili  mbali ya kufanyabiashara hizi kila siku, litaendelea kubaki masikini bila mafanikio yoyopte endapo serikali haitachukua mkakati wa maksudi kuhakikisha wananchi hawa wanapatiwa mafunzo ya namna ya kuendesha na kuendeleza biashara zao.

Serikali na wadau wengine wanapaswa kutambua kuwa kundi hili ni watu wenye vipato vidogo na vya kati ambao hawaweza kulipa maelfu ya pesa kugharamia mafunzo ya uendeshaji biashara.

Kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, sasa serikali ibuni mkakati wa maksudi kwa kushirikisha wadau wengine kuhakikisha inaandaa mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji shughuli za ujasiriamali mijini na vijijini bure.

Kwa kufanya hivyo, italeta mwamko kwa wadau hao kujua namna ya kuendesha shughuli zao na kuwapa ubunifu zaidi wa biashara mpya, tofauti na sasa ambapo ubunifu wa biashara hususan mijini uko chini sana.

Kila mtu anafanya biashara kwa kumwiga mwenzake, utakuta kila mahali biashara ni saloon, grosari, maduka ya dawa, chakula na nguo, tujiulize hivi hizi ndizo huduma pekee wanazohitaji wananchi? Sisi tunasema wafanyabiashara ndogo sasa wasaidiwe kupata elimu ya kuendeleza biashara zao.  


       

No comments:

Post a Comment