19 March 2012

Simba 'airforce one'

*Yaichapa Mtibwa 2-1*Azam yarudi penyewe

Na Elizabeth Mayemba, Morogoro
Simba inazidi kupasua anga kama ndege aina ya Airforce one!ndivyo unavyoweza kusema baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mechi ya ugenini iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Mabao ya Simba yaliyoifanya izidi kupasua anga katika msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 47 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 44 baada ya kuifunga Ruvu Shooting bao 1-0 jana, yalifungwa na Patrick Mafisango na Felix Sunzu.

Kwa ushindi huo, Simba imeendelea kujichimbia kileleni huku ikifuatiwa na Azam ambapo zote zimecheza michezo 21 na nafasi ya tatu inakamatwa na Yanga yenye pointi 43 na mchezo mmoja mkononi.

Katika mechi hiyo ya jana, iliyopigwa Morogoro, wenyeji Mtibwa walikuwa wa kwanza kubisha hodi langoni mwa Simba dakika ya tatu kupitia kwa Hussein Javu baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa Juma Kaseja na mabeki kuondosha hatari.


Simba ilijibu shambulizi hilo, dakika ya 15, kupitia kwa Shomari Kapombe ambaye alipiga shuti kali nje ya eneo la hatari lakini lilipaa juu ya goli.

Kiungo Patrick Mafisango wa Simba, aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 19, akimalizia vizuri pasi iliyopigwa na Emmanuel Okwi.

Mtibwa ilijitahidi kucheza kwa kasi ili kusawazisha na dakika ya 30, Javu tena akiwa katika nafasi ya kufunga alipiga shuti lililopaa juu ya goli na kufanya dakika 45 za kwanza Simba kuwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa Mtibwa kucheza kwa kasi na kusawazisha dakika ya 52, bao lililofungwa na Javu kutokana na mabeki wa Simba kufanya uzembe kwa kushindwa kuondosha hatari haraka langoni mwao.

Simba ilitulia na kufanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa Mtibwa na dakika ya 59, walipata penalti baada ya Salum Swed kumkwatua Okwi ndani ya eneo la hatari na Mafisango alipiga penalti hiyo na kukosa baada ya kipa Deogratius Munishi 'Dida' kuokoa.

Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Mathew Akrama, ambapo Mafisango mara ya kwanza alipiga na kukosa mwamuzi alidai kipa Dida alitoka kabla ya kuruhusiwa na kurudia tena ambapo Dida aliokoa.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu ambapo dakika ya 79, Sunzu aliwainua mashabiki wa Simba vitini kwa kufunga bao la pili kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Okwi

Naye Mwandishi Wetu, Speciroza Joseph anaripoti kwamba, timu ya Azam FC imeendelea kujiweka pazuri katika nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Bao pekee la Azam lilifungwa dakika ya 50 na mshambuliaji Mrisho Ngassa aliyeingia badala ya Ibrahim Mwaipopo na kuifanya timu hiyo irudi katika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 44 nyuma ya vinara wa ligi hiyo, Simba yenye pointi 47.


Katika mechi nyingine iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Mwandishi Wetu Daud Magessa anaripoti, kwamba wenyeji Toto African wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Dodoma katika mechi iliyokuwa na ushindani.

Toto ilikuwa ya kwanza kufunga bao lililofungwa na Eric Mulilo kwa mpira wa adhabu ndogo na Polisi walisawazisha dakika ya 48 kupitia kwa Juma Juma.

Mchezaji Kete Paul wa Toto aliisaidia timu yake kuibuka na pointi tatu baada ya kufunga bao kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 89 baada ya mchezaji mmoja wa toto kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Mtibwa: Deogratius Munishi, Juma Jaffar, Issa Issa, Salvatory Ntebe/Dickson Daud, Salum Swed, Shaaban Nditi, Ally Ally, Said Bahanuzi, Hussein Javu na Vicent Salamba/Said Mkopi.

Simba: Juma Kaseja, Derrick Walulya/Obadia Mungusa, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Juma Nyosso, Jonas Mkude, Salum Machaku/Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisango, Felix Sunzu, Haruna Moshi 'Boban' na Emmanuel Okwi.



No comments:

Post a Comment