19 March 2012

KNCU watoa bima ya afya kwa wakulima

Na Florah Temba, Kilimanjaro
WAKULIMA wa kahawa zaidi ya 1,700 kutoka katika Kijiji cha Mrimbo Uuwo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wameanza kupatiwa matibabu kupitia mpango wa Bima  ya Afya unaoratibiwa na Chama Kikuu cha Msingi cha Ushirika mkoani humo (KNCU), kwa ufadhili wa Uholanzi kupitia Shirika la Pharm Access.

Chama hicho kwa kushirikiana na wafadhili hao pia wameboresha huduma za afya na kusambaza misaada ya vifaa na dawa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa wahusika ikiwa ni pamoja na kukarabati majengo.
Hayo yalibainishwa na Mratibu wa Bima ya Afya KNCU, Bw. Yusuph Tumaini wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea Zahanati ya Uuwo na hospitali mbalimbali zilizofikiwa na mpango huo ikiwemo Hospitali ya Kilema mkoani humo, mwishoni mwa wiki. Bw.Tumaini alisema, katika ukarabati wa majengo kupitia mpango wa bima ya afya KNCU wametumia zaidi ya sh. milioni 40 kwa ajili ya ukarabati wa Zahanati ya Uuwo lengo likiwa ni kuboresha utoaji huduma.
Alisema, mpango huo unalenga kutoa huduma kwa wanachama wa chama hicho na familia zao katika hospitali, vituo vya afya na zahanati za serikali zikiwemo binafsi na kwamba Serikali ya Uholanzi inalipia sehemu ya gharama za bima ili kufanya ziwe nafuu na kuweza kulipwa kwa wakulima wote. Alisema, kwa sasa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanachama kutolipa ada zao kwa wakati ambapo alisema kunahitajika elimu ya kina ili wanachama waweze kuelewa umuhimu wa bima na faida zake.
Baadhi ya wanachama wanaonufaika na mpango huo wakizungumzia hatua hiyo waliipongeza KNCU na kuomba mpango huo uboreshwe ili kuweza kutoa huduma nzuri zaidi ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia wakulima ambao wengi wao wanatoka katika familia duni zisizo na uwezo.

No comments:

Post a Comment